Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba bado wawili ianze kunoga, Mbrazil yumo

Muktasari:

  • Leo na kesho Mwanaspoti limepenyezewa zinatatambulishwa mashine nyingine kali akiwamo beki kisiki kutoka Cameroon, Che Fondoh Malone na kipa Mbrazili, Caique Luiz Santos da Purificacao

Klabu ya Simba jana imekamilisha usajili wa winga Aubin Kramo kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili na anauwezo wa kucheza nafasi tatu tofauti uwanjani ikiwemo winga zote mbili na namba 10.

Winga huyo anayemudu kutumia miguu yote kwa ufasaha aliwahi kuwadhuru Simba mara mbili ambapo msimu wa juzi wekundu hao walipokutana na ASEC alihusika kwenye mabao mawili ya kwanza ya timu yake katika mechi mbili za nyumbani na ugenini.

Simba  hadi sasa imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji raia wa Cameroon, Leandre Willy Onana akitokea Rayon Sports ya Rwanda, kocha wa makipa, Mhispania Daniel Cadena aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam ili kuchukua nafasi ya Chlouha Zakaria Mbrazil kutoka Morocco, kisha kufuatia na kocha wa viungo Corneille Hategekimana aliyewahi kufanya kazi na Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' katika klabu ya Rayon Sports ya Rwanda sambamba na Mkenya Michael Igendia aliyeazimwa na Taifa Stars kutoka klabu ya Gor Mahia ya Kenya.

Leo na kesho Mwanaspoti limepenyezewa zinatatambulishwa mashine nyingine kali akiwamo beki kisiki kutoka Cameroon, Che Fondoh Malone na kipa Mbrazili, Caique Luiz Santos da Purificacao ambao wanaifanya Simba ikamilike na kumpa kazi nyepesi kocha Robertinho anayekuwa na kikosi imara kinachoweza kushiriki michuano yoyote bila presha tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita wakikosekana baadhi ilikuwa majanga.

Usajili wa kipa kutoka Brazili, Caique umeifanya Simba kuwa na uhakika wa uimara langoni kwa muda wote ambao kipa chaguo la kwanza, Aishi Manula atakuwa anauguza majeraha yake baada ya kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini.

Hii inamaanisha kuwa Ally Salim aliyemalizia mechi za mwishoni za msimu uliopita, atakuwa na jukumu la kumsaidia Purificao ikiwa mambo yataenda kama yalivyopangwa, huku chipukizi Feruzi Teru akiwa kama silaha ya akiba.

Katika safu ya ulinzi, beki Joash Onyango inatajwa kuwa anaomba kuondoka, lakini usajili wa Che Fondoh Malone unawapa jeuri Simba ya kumpa mkono wa kwaheri Mkenya huyo ambaye tetesi zinadai kuwa anajiandaa kujiunga na Singida Fountain Gate.

Ukuta wa Simba haujabomoka sana, kwani mabeki wa pembeni, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein 'Tshabalala' wote wamebakia kikosini kama ilivyo kwa mabeki wa kati, Enock Inonga na Kennedy Juma.

Pamoja na kuondokewa na viungo wawili wa ulinzi yaani, Jonas Mkude anayetajwa kujiandaa kutua Yanga na Erasto Nyoni aliyesajiliwa Namungo, Simba haina haraka sana ya kusaka wachezaji wa kucheza katika nafasi hiyo kwani Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute bado wapo kikosini hivyo jukumu lililopo kwa Simba hivi sasa ni kusaka mchezaji/wachezaji watakaoongeza nguvu eneo hilo.

Baada ya Augustine Okrah kuondoka, Simba imefanya uamuzi wa haraka wa kumsajili winga wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Aubin Kramo aliyetambulishwa jana saa saba mchana huku ikiwa imemnasa mshambuliaji Mcameroon Willy Onana kutoka Rayon Sports ambaye anamudu pia kucheza nafasi ya winga, huku Fabrice Ngoma naye anatajwa kupewa mkataba mmoja na kilichosubiriwa kwa sasa ni kutambulishwa tu.

Kama haitoshi, Simba pia imefanikiwa kubaki na kiungo fundi, Saido Ntibazonkiza anayemudu kucheza nafasi ya winga pamoja na mawinga wengine, Kibu Denis, Pape Ousmane Sakho na Jimmyson Mwanuke.

Nafasi ya kiungo mshambuliaji yupo Clatous Chama akisaidiwa na kiraka Nassor Kapama ambaye anamudu kucheza kama beki, kiungo mkabaji na mshambuliaji akiwa amebakishwa kikosini lakini kwa mshambuliaji wa kati, Simba ina Jean Baleke sambamba na Mohammed Musa na John Bocco.

Kutokana na wachezaji alionao hadi sasa, kocha Robertinho anaweza kuanza msimu na kikosi kinachoundwa na Caique Luiz Santos da Purificao, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Enock Inonga, Che Fondoh Malone, Sadio Kanoute, Willy Onana, Mzamiru Yassin, Jean Baleke, Clatous Chama na Aubin Kramo.
Kwa upande wa kikosi cha akiba Simba inaweza kuwa na Ally Salim, Israel Mwenda, Kennedy Juma, Kibu Denis, Saido Ntibazonkiza, Jimmyson Mwanuke, Nassor Kapama na Pape Sakho.


WASIKIE WADAU
Beki na nahodha wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa amesema kuwa timu hiyo inahitaji maingizo machache kikosini.
"Simba ina kikosi kizuri inapaswa tu kuongeza wachezaji kwenye baadhi ya maeneo kama vile beki wa kati, kiungo na mshambuliaji. Wakija wachezaji wazuri kwenye maeneo hayo, timu yao itaimarika zaidi.
"Ukitazama msimu uliomalizika changamoto kubwa ilikuwa ni kutokuwa na kikosi kipana tu lakini kile kilichokuwa kinaanza kilikuwa ni kizuri," alisema Pawasa.
Kocha wa zamani wa Coastal Union, Joseph Lazaro alisema, Simba inapaswa kuwa na utulivu hasa kwa usajili wa wachezaji wa kigeni.
"Na sio Simba tu bali timu zote nyingine zinatakiwa kusajili wageni ambao wataongeza kitu katika vikosi vyao. Simba ni miongoni mwa timu bora hivyo hata usajili wao hautakiwi kufanywa mkubwa," alisema Lazaro.