Shaqiri azidi kumuharibia Mourinho
Muktasari:
- Mabao mawili ya haraka haraka dakika ya 73 na 80 kutoka kwa mtokea benchi Xherdan Shaqiri, sio tu kwamba yaliipa Liverpool ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester United, bali yamekiweka rehani kibarua cha kocha Jose Mourinho, ambapo yameibua upya hasira za mashabiki wa timu hiyo
Liverpool, England. Mchezaji Xherdan Shaqiri jana alitoka benchi na kuifungia Liverpool mabao mawili katika ushindi 3-1 dhidi ya Manchester United kwenye Uwanja wa Anfield, akizidi kumuweka katika wakati mgumu kocha Jose Mourinho.
Wakati mchezaji huyo anaingia uwanjani matokeo yalikuwa 1-1baada ya Sadio Mane kufunga dakika ya 24 na Jesse Lingard akasawazisha dakika ya 33 na kudumu hadi mapumziko lakini mtokea benchi Shaqiri ndiye aliyeharibu kila kitu kwa kufunga mabao yake dakika ya 73 na 80.
Hasira za mashabiki wa Man United kwa kocha huyo zimewaka upya na sasa wanataka atimuliwe, huku baadhi ya wadau wengine nao wakiwemo wachambuzi wakiunga mkono hoja ya mashabiki.
Wengi wao wanaamini kuwa kocha huyo hana uhusianao na mshikamano mzuri na wachezaji wake wengi ndio maana timu inashindwa kufanya vizuri.
Man United imebaki katika nafasi ya sita lakini imepitwa kwa pointi 26 na vinara wa Ligi hiyo Liverpool, pengo ambalo kipa wa zamani wa Real Madrid na Hispania, Iker Casillas, alisema iwapo ataendelea kubakia atazidi kuigharimu timu hiyo.
Iker alisema Mourinho anazidi kuthibitisha kuwa mafanikio yote aliyoyapata yalitokana na juhudi za watu wengine alioshirikiana nao na ndio maana hakuwa akidumu katika timu ili kuficha udhaifu wake.
Kipa huyo alikwaruzana na Mourinho wakati wapo Madrid mwaka 2013 baada ya kocha huyo kumuweka benchi katika mechi nyingi na baadaye kupendekeza auzwe.
Baadahi ya mashabiki walihoji sababu za msingi za kumuweka nje kiungo Paul Pogba, kiungo ambaye akiingia uwanjani anasaidia kupatikana matokeo mazuri licha ya kuwa na msuaguano wa kila mara na kocha huyo.
Kipigo hicho kimeiacha Man United bila ya wastani wa mabao ikifunga na kufungwa 29 ukiwa na wastani wa chini zaidi katika historia ya klabu hiyo kwa mechi 17 za mwanzo tangu msimu wa 1990-91.
Akiuzungumzia mchezo huo Mourinho alijibu kwa kifupi kuwa timu bora imeshinda, ukiwa ushindi wa kwanza mkubwa kwa Liverpool kwenye Uwanja wa Anfiled tangu Machi 2011 walipoishinda Man United kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Hoja ya mashabiki wanaotaka kocha huyo atimuliwe imejikita katika rekodi wakisema ni mara ya kwanza kufungwa mabao mengi namna hiyo mwanzoni mwa msimu mara ya mwisho kuwa na matokeo mabaya namna hiyo ilikuwa msimu wa 1962-63.
Mchezaji Shaqiri amekuwa mchezaji wa pili wa Liverpool kufunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza kucheza dhidi ya Man United wa kwanza alikuwa mshambuliaji Nigel Clough, aliyefanya hivyo Januari 1994.
Mwandishi wa habari wa BBC, Phil McNulty, alisema kwa namna mashabiki wa Man Unityed wanavyozungumza itakuwa vigumu kumuona Mourinho kwenye timu hiyo msimu ujao.