Tanzania yaanza kupigania medali Jumuiya ya Madola
Muktasari:
- Mashindano hayo yanayoanza leo hadi Agosti 1 2026, yanawashirikisha mabondia 201, wakiwemo wanaume 131 na wanawake 70, kutoka mataifa 43 ya Jumuiya ya Madola, wakishindana katika uzani 14 tofauti.
TIMU ya ngumi ya ridhaa ya Tanzania, leo itaanza safari ya kutafuta medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka 2026, ambapo mabondia watatu wataingia ulingoni katika ukumbi wa Scottish Event Campus (SEC) jijini Glasgow.
Ratiba rasmi ya droo imeipa Tanzania mechi ngumu za mwanzo dhidi ya wapinzani kutoka Nigeria, Zambia na Lesotho, huku mashindano ya ngumi yakianza rasmi.
Mashindano hayo yanayoanza leo hadi Agosti 1 2026, yanawashirikisha mabondia 201, wakiwemo wanaume 131 na wanawake 70, kutoka mataifa 43 ya Jumuiya ya Madola, wakishindana katika uzani 14 tofauti.
Anayeongoza kampeni ya Tanzania katika uzani wa light heavyweight (kilo 80) kwa wanaume ni Yusuf Changalawe ambaye atapambana na Ankintola David wa Nigeria katika hatua ya raundi ya 32.
Bondia mwingine wa Tanzania, Faki Issa Faki, naye ataanza kampeni yake katika uzani wa bantamweight (kilo 55) kwa wanaume kwa kumenyana na Mwengo Mwale wa Zambia katika hatua ya raundi ya 32.
Hata hivyo, matumaini makubwa ya Tanzania ya kupata medali mapema yanaelekezwa kwa Zawadi Kutaka, maarufu kama "Malkia wa Tanzanite".
Bondia huyo wa uzani wa featherweight (kilo 57) tayari amefuzu moja kwa moja hadi hatua ya robo fainali baada ya kupita bila kupigana katika raundi ya kwanza (bye), hivyo anahitaji ushindi mmoja tu ili kujihakikishia nafasi ya kushindania medali.
Katika pambano lake la kwanza atakutana na bondia kutoka Lesotho.
Kutaka tayari ameandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanzania kuiwakilisha nchi katika mchezo wa ngumi kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, jambo linaloongeza umuhimu wa ushiriki wake jijini Glasgow.
Mbali na ngumi, Tanzania pia inawakilishwa katika michezo mingine mitatu kwenye mashindano hayo.
Riadha ndiyo mchezo wenye idadi kubwa zaidi ya wawakilishi wa Tanzania, ambapo wanariadha sita wanatarajiwa kuanza mashindano yao siku ya Jumatatu, Julai 27, wakati mbio na mashindano ya uwanjani yatakapoanza katika Uwanja wa Scotstoun.
Aidha, Tanzania itawakilishwa na wachezaji wawili wa judo, ambao watashiriki mashindano yatakayofanyika kuanzia Julai 31 hadi Agosti 2 katika ukumbi wa SEC.
Mwogeleaji Collins Saliboko naye atashiriki mashindano ya kuogelea katika Tollcross International Swimming Centre, ambapo mbio za kuogelea zinaanza leo.