Serengeti Boys yaanza AFCON U-17 na ushindi, yaongoza kundi
Muktasari:
- Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote mbili zikionyesha nia ya kushambulia katika dakika za mwanzo. Msumbiji ilijaribu kushambulia mapema, lakini Tanzania ilianza kutulia taratibu na kuonekana kuwa hatari zaidi mbele ya lango.
TANZANIA imeanza vyema kampeni yake ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2026 (AFCON U-17) baada ya kuifunga Msumbiji mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi C uliochezwa leo Mei 14, 2026 kwenye Uwanja wa Mohammed VI Football Academy Pitch 11 nchini Morocco.
Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote mbili zikionyesha nia ya kushambulia katika dakika za mwanzo. Msumbiji ilijaribu kushambulia mapema, lakini Tanzania ilianza kutulia taratibu na kuonekana kuwa hatari zaidi mbele ya lango.
Kikosi hicho cha vijana wa Tanzania maarufu Serengeti Boys, kilipata bao la kwanza dakika ya 26 kupitia mshambuliaji Dismas Athanasi.
Mchezaji huyo alipokea mpira nje kidogo ya eneo la penalti kabla ya kupiga shuti kali lililojaa wavuni. Bao hilo lilihakikiwa kwanza na mfumo wa VAR kabla ya kuthibitishwa rasmi, jambo lililosababisha shangwe kubwa kwa wachezaji na benchi la Serengeti Boys.
Serengeti Boys iliongeza bao la pili dakika ya 35 baada ya kosa kubwa la beki wa Msumbiji, Pascoal Demi. Beki huyo alijaribu kumrudishia mpira kipa João Jofrisse, lakini ulimpita na kuingia wavuni na kuwa bao la kujifunga.
Baada ya mapumziko, makocha wa timu zote walifanya mabadiliko kadhaa ya kimkakati, lakini kocha wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu, ndiye ambaye mabadiliko yake yalionekana kuwa na faida kubwa zaidi.
Dakika ya 63, Razaki Mbengelendi aliifungia Serengeti Boys bao la tatu kwa kichwa kizuri kilichohitimisha ushindi muhimu kwa vijana hao na kuonyesha ubora wao wa kushambulia.
Ushindi huo umeifanya Serengeti Boys kufikisha pointi tatu na kuongoza Kundi C. Mali na Angola zina pointi moja kila moja baada ya kushindwa kufungana mapema leo.
Serengeti Boys sasa itaelekeza nguvu zake kwenye mchezo wa pili wa hatua dhidi ya Angola utakaochezwa Mei 17, 2026 saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Serengeti Boys iliwasili Morocco ikiwa na dhamira ya kuweka historia kwa kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kufanya hivyo katika mashindano ya mwaka 2017, 2019 na 2025, ambapo iliishia hatua ya makundi.
Kutokana na kuongezeka kwa nafasi za kufuzu Kombe la Dunia la FIFA kwa vijana chini ya miaka 17 kwa timu za Afrika, Serengeti Boys itakuwa na matumaini ya kujitangaza kama moja ya mataifa mapya yanayochipukia kisoka barani Afrika.
Mwanzo huo mzuri dhidi ya Msumbiji, tayari umetuma ujumbe wa matumaini kuwa Tanzania inaweza kuwa moja ya timu zitakazokuja kushangaza wengi katika mashindano hayo.