Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SCUD WA YANGA: Kiboko ya Simba sasa mfugaji wa kisasa-1

Said Sued

Muktasari:

Vita hiyo ilikuja baada ya Iraq iliyokuwa ikiongozwa na Saddam Hussein kuivamia Kuwait, ndipo Marekani ilipoongoza mashambulizi dhidi ya majeshi ya Iraq

SIKU zinakwenda na maisha yanasonga mbele na historia inazidi kubadilika. Ni miaka zaidi ya 20 imepita sasa tangu mabomu aina ya Scud yawe gumzo duniani wakati wa Vita ya Ghuba, vita ambayo Marekani na washirika wake waliishambulia Iraq miaka ya 1990 mwanzoni.

Vita hiyo ilikuja baada ya Iraq iliyokuwa ikiongozwa na Saddam Hussein kuivamia Kuwait, ndipo Marekani ilipoongoza mashambulizi dhidi ya majeshi ya Iraq.

Ni wakati huo ambao jina la Scud lilipamba moto, kila kitu chenye nguvu au mafanikio kilifananishwa na Scud na mashabiki wa Yanga walimbatiza jina la Scud mshambuliaji wao wa enzi hizo, Said Sued.

Said Sued alibatizwa jina hilo baada ya kuiliza Simba kila mara walipokutana na timu hiyo, leo hii ukiwatajia jina hilo mashabiki wa enzi hizo wa Yanga utakuwa umewakumbusha mmoja wa washambuliaji wao mahiri.

Mwanaspoti lilitua mkoani Kigoma na kukutana na Scud ambaye sasa anajishughulisha na shughuli za ufugaji ng’ombe wa kisasa pamoja na ukulima.

Scud bado ni maarufu mkoani Kigoma, anaishi maeneo ya Mwanga, Kigoma Mjini mahali ambako pia amejenga nyumba yake ingawa ukimuona Scud wa sasa unaweza kumshangaa kidogo kutokana na mzuzu (ndevu za kidevuni) alizofuga.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Scud hakusita kufafanua kwamba ndevu hizo ni suna kutokana na imani ya dini yake ya Kiislamu lakini pia Scud wa sasa ana alama nyeusi kubwa juu ya paji lake la uso (sijda).

Mambo hayo mawili ni uthibitisho kwamba Scud wa sasa ni mtu wa ibada, ni muumini wa dini ya Kiislamu, muumini ambaye kwa mtazamo wa haraka unaweza kujiaminisha kwamba anaswali swala tano.

Baada ya kuwasiliana na Scud na kumpa taarifa za ujio huo, mchezaji huyo akamtuma kijana mwendesha pikipiki ili akampokee mwandishi kwenye Kituo cha Mabasi cha Mwanga maarufu kwa Mchaga hadi nyumbani kwa Scud, maeneo ya Mwanga Kisangani B.

Scud alikutwa na mwandishi akiwa amejipumzisha nje ya nyumba yake kwenye kibaraza, nyumba ambayo anaishi yeye, mkewe (amekataa kumtaja jina) pamoja na watoto wake.

Nje ya nyumba yake, kumezungukwa na mazizi ya ng’ombe, pembezoni wapo bata na kuku wachache mambo ambayo yanatoa uthibitisho kwamba mwenye mji huo ni mfugaji.

“Karibu, hapa ndiyo nyumbani kwangu, baada ya kustaafu maisha ya mpira ambayo kama unavyojua yalikuwa ni kuhamahama, nikajihifadhi hapa,”anasema Scud.

“Nipo naishi na familia yangu mke wangu (anamwita atoke ndani na kumtambulisha kwa mwandishi) pamoja na watoto wangu ingawa wengine wako masomoni.

“Karibu kwetu Kigoma, kuna changamoto, mitihani ya hapa na pale na mambo mengine mengi tu, tupo na mji wetu ili mradi mkono unakwenda kinywani,”anasema Scud huku akitabasamu.

Alivyotua Yanga

Baada ya mazungumzo hayo, Scud alianza kuelezea maisha yake ya soka hadi kutua Yanga na hali anavyoiona sasa.

“Huwa nafarijika sana ninapozungumza maisha ya mpira hapo nyuma, nilipotoka nyumbani Kigoma hadi Dar es Salaam na kusajiliwa na Yanga,”anasema.

Anasema, historia yake ya soka ilianza tangu alipokuwa mdogo anasoma Shule ya Msingi Furahisha sasa Mwenge iliyopo Mwanza na baadaye alirudi Kigoma na kumaliza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Katubuka.

Wakati huo huo, alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa mashindano ya wanafunzi wa shule za msingi maarufu Umitashumta mwaka 1986 mjini Arusha na mwaka 1988 mjini Songea akitokea timu ya Mkoa wa Kigoma.

Baada ya mashindano hayo, alisajiliwa na Klabu ya NBC Kigoma na mwaka 1990, wakaenda kushiriki mashindano ya sherehe za kuzima Mwenge mkoani Tabora na katika mashindano hayo anakumbuka Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alikuwa mgeni rasmi.

Scud anasema, hawezi kusahau mchezo huo ambao walifanikiwa kuchukua ubingwa baada ya kuifunga Kurugenzi Tabora bao 1-0 bao ambalo mfungaji alikuwa yeye.

“Mechi hiyo ilinitambulisha zaidi na tuliporudi Kigoma tu, ndiyo mpango wa usajili wa Yanga ulipoanza. Nakumbuka niliitwa Kasulu na mzee mmoja anayeitwa Arif Aziz, huyo ndiye aliyenisainisha mkataba wa mwaka mmoja.

“Baada ya kusaini mkataba ule nilipewa Sh 100,000 na enzi hizo zilikuwa fedha nyingi,”anasema Scud ingawa hajui pesa hizo alizitumia kwa kufanya kitu gani kwani nyumba anayoishi sasa aliijenga kwa pesa tofauti na mpira.

Akumbuka alivyowaliza Simba

Historia ya kuwafunga Simba katika mechi hizo mbili za Ligi Daraja la Kwanza mwaka 1991 bado haijavunjwa na mchezaji mwingine. Yanga ilishinda bao 1-0 mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Mei 18 na mechi ya pili ya mzunguko wa pili Yanga ilishinda kwa bao 1-0 Agosti 31.

“Nilikuwa mchezaji mzuri lakini sikuwa na uzoefu kwani ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kucheza mechi kubwa kama hiyo lakini kwa sababu nilipenda kufunga, niliingia uwanjani nikiwa nimejiamini,”anasema Scud.

“Mechi ya kwanza nakumbuka, nilifunga dakika ya sita na pasi nilipewa na Issa Athuman Mgaya (marehemu). Katika mechi hiyo kipa wa Simba alikuwa Iddi Pazzi.

“Mechi ya pili, bao lilitokana na mpira wa kona uliopigwa ndani ya 18, sikumbuki dakika, lakini nilipofunga tu nilitoka na aliingia Joseph Machela.

Ajabu, atimka Yanga

Unaweza kushangaa kwani licha ya kufanya maajabu hayo, Scud alicheza msimu huo mmoja tu Yanga na ulipomalizika alikwenda kuichezea Milambo ya Tabora aliyodumu nayo kwa miaka mitano.

Itaendelea Jumanne ijayo...