Prime
Sapraizi nyingine Simba Day, kushusha kipa
KLABU ya Simba katika kuadhimisha tamasha lao la Simba Day leo Jumamosi Agosti 8, 2026, imekuja na sapraizi kwa mashabiki wake ikiwa na mpango wa kumtambulisha kipa mpya.
Simba Day inayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1936, kutakuwa na burudani mbalimbali huku tukio la mwisho ni la kucheza mechi ya kirafiki ambapo Simba itaikabili Kenya Police.
Kabla ya mechi hiyo, kunafanyika zoezi la utambulisho wa wachezaji watakaotumika kwa msimu ujao wa 2026-2027 ambapo ndani ya utambulisho huo, ndipo kuna sapraizi.
Mwanaspoti limepata taarifa kutoka kambi ya Simba kwamba, klabu hiyo imemsajili golikipa namba moja wa JKU ya Zanzibar, Ahmed Issa, atakayeungana na Mahamadou Kassali na Hussein Abel.
Chanzo hicho kilisema ujio wa kipa huyo katika kikosi hicho ni kutokana na Yakoub Suleiman ambaye msimu wa 2025-2026 alitua Simba akitokea JKT Tanzania, hakuwa na wakati mzuri baada ya kuumia na kufanyiwa upasuaji uliomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
"Ni kipa mzuri, hivyo atasaidiana na waliopo, ambao ni kipa mgeni Mahamadou Kassali, na mzawa mwingine Hussein Abel," kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Usajili wake umezingatia uwezo wake alioonyesha msimu uliopita katika Ligi ya Zanzibar, pia tunategemea Yakoub akipona basi atarejea katika majukumu yake."
Yakoub kabla ya kutua Simba, msimu wa 2024-2025 akiwa JKT Tanzania alionyesha kiwango kizuri akimaliza na cleansheets nane za Ligi Kuu Bara.
Kipa huyo mpya anayetarajiwa kutambulishwa leo, msimu uliopita akiwa na JKU katika Ligi Kuu Zanzibar, alimaliza na cleansheet 10, nyuma ya kinara Hamad Ubwa aliyekuwa Mlandege na cleansheet 12. Pia aliwahi kupata tuzo ya golikipa bora wa mashindano ya Kombe la Muungano mwaka 2025.
Kassali ndiye kipa namba moja wa Simba ambapo alitua kikosini hapo dirisha dogo la Januari 2026, akafanikiwa kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara 2025-2026 alimaliza na cleansheets 16, nyuma ya kinara Djigui Diarra wa Yanga aliyekuwa na 18.
Hadi sasa, Simba imetambulisha nyota wapya sita ambapo watatu wa kimataifa ni winga raia wa Afrika Kusini, Keletso Makgalwa, kiungo Mnigeria, Ibraheem Jabaar na mshambuliaji Ibrahim Doumbia raia wa Mali, huku wazawa ni viungo Kelvin Nashon na Bakari Msimu, pia beki Nathaniel Chilambo.