Mzuka wa mashabiki Simba Day, Yanga nao wamo
Muktasari:
- Mwanaspoti lipo live kukuletea matukio mbalimbali yanayoendelea katika tamasha hilo, ambapo nje zinaendelea shughuli tofauti kama burudani, biashara na wengine wakiwa katika mstari wa foleni ya kuingia ndani.
LEO Agosti 8, 2026 ni kilele cha tamasha la Simba Day, linalofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, hali ya mashabiki wa Simba ilivyo ndani na nje, ni kubwa, huku wengine hamu yao ikiwa ni kuona nyota wao wapya. Miongoni mwa mashabiki waliopo ni kutoka kwa watani wao wa jadi, Yanga.
Mwanaspoti lipo live kukuletea matukio mbalimbali yanayoendelea katika tamasha hilo, ambapo nje zinaendelea shughuli tofauti kama burudani, biashara na wengine wakiwa katika mstari wa foleni ya kuingia ndani.
Wapo mashabiki wanaoingia ndani, huku wengine wakiangalia burudani kwa muziki unaopigwa nje ya eneo la Uwanja wa Uhuru.
Klabu hiyo ikiwa imetimiza miaka 90 tangu ilipoanzishwa mwaka 1936, inakuwa mara ya pili kufanya tamasha hilo katika Uwanja wa Uhuru. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009, chini ya aliyekuwa mwenyekiti, Hassan Dalali.
Ukiachana na mashabiki hao, usalama upo imara kila kona, askari wakifanya kazi ya kuelekeza watu, huku wengine wakizunguka kuona kila kitu kinakwenda sawa.
Miongoni mwa mashabiki ambao wametoa maoni yao kuhusiana na tamasha hilo, alijitambulisha kwa jina la Ally Omary ambapo amesema: "Nitawaona wachezaji wapya na aina ya uchezaji wao katika mechi ambayo Simba tunacheza na Polisi ya Kenya."
Mwingine aliyechangia hilo amejitambulisha kwa jina la Sabi Ndomba, amesema: "Ninapata nafasi ya kushuhudia wachezaji wa Simba na kuona taswira ya msimu mzima."
Kama unavyojua Simba mtani wake ni Yanga, shabiki wa timu hiyo yenye maskani yake Jangwani aliyejitambulisha kwa jina la Cosmas Komba, amesema: "Kuna ubaya gani kuja kushuhudia shughuli ya mtani, lakini wasubiri kesho wataona majembe ya Yanga, kuna Allan Okello, Shalulile yaani ni mwendo wa burudani na kicheko."