Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samatta anatuzalishia kina Diamond Platinumz wengi

Muktasari:

Best alikuwa kielelezo cha mchezaji mwenye kipaji na mpenda starehe. Kuhitimisha jinsi gani alizipenda starehe kuna mambo mawili unaweza kuyasema. Kwanza alitembea na Miss World wanne. Pili, mpira ulimshinda akiwa na miaka 28 tu.

DUNIA imebadilika sana. Kabla ya Cristiano Ronaldo kutamba katika ulimwengu wa ubishoo na soka, zamani Waingereza walikuwa na mtu anaitwa George Best. Kipaji maridhawa cha soka. Waingereza walimwita ‘Belfast Boy’ kwa sababu alikuwa anatoka katika Mji Mkuu wa Ireland Kaskazini, Belfast.

Best alikuwa kielelezo cha mchezaji mwenye kipaji na mpenda starehe. Kuhitimisha jinsi gani alizipenda starehe kuna mambo mawili unaweza kuyasema. Kwanza alitembea na Miss World wanne. Pili, mpira ulimshinda akiwa na miaka 28 tu.

Baada ya miaka mingi akaja Ronaldo. Wakati ule anachezea wasichana kabla ya kuamua kutulia kwa sasa. Ana watoto wanne kwa sasa na anaonekana ametulia. Ronaldo, mpaka sasa ana sifa ya kuonekana kuwa mwanasoka mwanamitindo. Mwanasoka mcheza filamu. Au Hollywood footballer.

Soka ni mchezo wa kigumu lakini siku hizi umekuwa mchezo laini kidogo, ndani na nje ya uwanja. Nje ya uwanja wanasoka wanaishi maisha yanayotamanisha. Wanaendesha magari ya kifahari, wanaishi kifahari.

Picha zao zinawaonyesha wakiwa katika magari yao ya kifahari, Limousine, Jaguar, Ranger Rovers na mengineyo. Wanaonekana wakiwa wamepiga picha katika ndege binafsi. Mavazi ya gharama yenye mvuto, na kila kitu ambacho kinawatamanisha raia wa chini.

Tanzania wapo vijana wanayoyaishi maisha haya. Sio wanasoka. Kuna kundi la kina Diamond Platinumz na wenzake wanaojiita Wasafi. Kuna kina Alli Kiba. Kuna wengineo. Katika soka hawapo watu wa namna hii. Mbwana Samatta angeweza kuwa katika kioo hiki.

Bahati mbaya au nzuri, Samatta sio mtu wa maisha haya. Anaendesha maisha yake kimyakimya sana. Ni mtu wa dini pia. Hapendi kuandikwa vibaya wala vizuri. Waandishi wa habari wanaambulia patupu pindi wanapojaribu kuchunguza kwa undani upande wa pili wa maisha ya Mbwana.

Kwa mfano, mshahara wake TP Mazembe ulikuwa siri. Mshahara wake wa sasa Genk umewaacha watu wakibashiri zaidi kuliko kuzungumza ukweli. Utajiri wake binafsi umebakia kuwa siri. Mtu mzima mmoja alininong’oneza ‘Huyu kijana kajenga jumba la ajabu kule kwetu Kigamboni’. Mwingine aliniambia ‘Samatta kanunua nyumba Upanga’.

Hivi ndivyo maisha ya Samatta yalivyo. Kibinadamu ni sahihi kabisa. Lakini mchezo wa soka umegubikwa na mambo mengi zaidi hasa nje ya uwanja. Kinachotokea kwa sasa ni rahisi kwa kijana mdogo mwenye kipaji cha soka kuamua kuwa Diamond kuliko Samatta. Sababu ni rahisi tu, aina ya maisha ambayo Diamond anaishi.

Bahati mbaya, staa wetu wa kwanza mkubwa wa soka katika zama mpya ni mkimya na mpole. Hana makeke. Inasaidia sana katika maisha binafsi ya soka kwa sababu wachezaji wetu wengi wenye mbwembwe hawafiki kokote. Wanaishia Uwanja wa Taifa tu.

Hata hivyo, haitusaidiii sana kuwapata kina Mbwana wengine. Kuna wachezaji wa Kitanzania najaribu kuwatazama nawaona wanamchukulia Mbwana kama mchezaji wa kawaida. Labda kwa sababu hasimulii anavyoishi, hasimulii anavyofaidi, hasimulii anacholipwa. Amekaa kimya.

Kama vijana wengi mjini wangejua Samatta anavyoishi wote wangeongeza juhudi mara tatu kwa ajili ya kufika alipo. Hata hivyo, si ajabu wengi kati yao wanatundika daluga juu na kuamua kwenda studio kwa ajili ya kujaribu kuwa Diamond. Ni kwa sababu maisha ya Diamond yamejaa mitandaoni.

Inapofikia hatua hii mimi kama mwandishi najaribu tu kuwakumbusha kwamba Samatta anaishi. Anaishi vema. Anaishi Kuliko wao wanavyofikiria. Nilikwenda Genk mwaka mmoja uliopita na katika apartment ambazo Samatta anaishi ni ndoto kwa zaidi ya familia asilimia 90 ya Watanzania kuziishi.

Katika Apartment tu za residentie Albert ambazo anaishi Samatta kama angekuwa anaishi Daimond ingekuwa habari kubwa zaidi nchini. Ama ni kwa yeye mwenyewe kutaka watu ajue, au ni kwa udadisi wa sisi wenyewe kutaka watu wajue.

Kama mfanyakazi wa Kizungu wa Samatta angekuwa ndiye mfanyakazi wa Diamond Platinumz nadhani ingekuwa habari nzito katika mitandao. Huyo Mzungu angechimbwa na lingeonekana jambo la ajabu kwa Diamond kuajiri Mzungu.

Mambo haya ndiyo ambayo ambayo yatasabaabisha vijana wengi waende studio kuliko katika viwanja vya soka vya mitaani kwao. Wengi watataka kuwa Diamond kuliko Samatta bila ya kujali ni kiasi gani Samatta anafurahia maisha kwa kiwango kikubwa, lakini kimya kimya.

Kuna marafiki zangu wamepita katika soka miaka michache iliyopita. Kama wao wangekuwa Samatta, si ajabu upepo ungekuwa tofauti. Nadhani kila kijana angetamani kukimbilia nje. Bahati mbaya walibeba sifa zao katika Uwanja wa Taifa na wamezizika sifa hizo hizo katika uwanja huohuo.

Hakuna unachoweza kumbadili Samatta awe tofauti na alivyoumbwa lakini pengine ni wakati wa kuweka wazi baadhi ya mafanikio yake binafsi ili vijana wavutike pia na maisha yake ya nje ya uwanja.

Nchi nyingi zilizoendelea kisoka zina mashujaa ambao vijana wengi waliyatamani maisha yao ya ndani na nje ya uwanja. Hasa nje ya uwanja. Mzazi hawezi kumruhusu mtoto wake kucheza soka hata kama yeye anashingilia soka, labda kama ajue kumbe wanasoka ni matajiri kuliko wasomi wengi tulionao.