Prime
Rasmi Dube apeleka mzigo wa kuvunja mkataba Azam FC

BAADA ya Mwanaspoti kuripoti kwamba mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ameandika barua kuomba kuvunja mkataba, klabu hiyo jana jioni ikatoka hadharani na kuthibitisha habari hiyo kupitia mkuu wa idara yake ya habari, Thabith Zakaria.
Katika taarifa ya video fupi iliyotolewa na klabu hiyo, Dube anatakiwa kulipa kiasi cha dola za Marekani laki tatu ambazo ni zaidi ya Sh700Milioni za Kitanzania.
Sasa kuna mpya. Staa huyo jana jioni amezungumza na viongozi na kuwaambia kwamba anaomba alipe dola 200,000 ambazo ni kama Sh510Milioni ili wamalizane aondoke zake kwenye viunga vya chamazi hivi karibuni.
Kiasi hicho cha fedha anachotaka kulipa ni kile ambacho Azam walimlipa mwaka jana wakati akaongeza mkataba huo mpya unaomalizika mwaka 2026.
Habari za ndani ya Azam ni kwamba bado kuna majadiliano yanaendelea kuhusiana na dau hilo pamoja na uamuzi wa mchezaji huyo huku wengine wakikereka kwanini amefanya jambo hilo wakati huu?
Lakini Mwanaspoti linajua kuwa sehemu kubwa ya Wakurugenzi wamekubaliana kwamba Dube aondoke wakikerwa na 'kitrendi' chake cha kuandika barua ghafla bila kusema chochote hapo kabla kama kuna jambo haliendi vizuri.
Wengi wao wanaona kama kaonyesha dharau kubwa na hakuna kingine zaidi ya kumruhusu aondoke ingawa bado ishu ya dau alilokuja nalo mezani bado halijafikiwa muafaka wowote mpaka muda huu.
Kuna vyanzo vitatu vinatajwa kama sababu ya yeye kuomba kuondoka, ikiwemo Yanga, Ihefu na timu za Zimbabwe, lakini vyanzo vya kuaminika vinasema kuna kitu kinaendelea kimyakimya njiapanda ya Jangwani.
YANGA
Wanahitaji sana huduma yake. Wanaamini Prince Dube anaweza kuwa mtu sahihi wa kuziba nafasi ya Fiston Mayele.
Inaaminika kwamba Yanga wamekuwa wakihangaika kumshawishi mchezaji huyo kwa muda mrefu kutua katika kikosi hicho kutokana na uwezo wake.
Hivi karibuni wakati Azam FC ikiwa mikoani kwa mechi za Ligi Kuu, Dube alionekana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akishuhudia mechi ya Yanga ambapo ilishinda mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad.
Dube hakusafiri na Azam kwa sababu ni majeruhi ambapo amekosa michezo kadhaa hadi sasa.
Nyota huyo hajacheza mechi ya Azam FC tangu Februari 19 alipoingia kipindi cha pili dhidi ya Tabora United.
Hakusafiri na timu katika mechi mbili za mikoani - Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons na Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate.
Lakini Mwanaspoti linajua kwa kawaida Azam FC husafiri na wachezaji wake hata kama ni majeruhi kama sehemu ya kujenga umoja. Hata hivyo, Dube hakusafiri ikisemekana alikataa kusafiri kama sehemu ya shinikizo ili aachwe huru.
Habari za ndani ni kwamba inasemekana kuna mfanyakazi mmoja wa Yanga ambaye hapo kabla alikuwa Azam ndiye anayechora ramani ya Dube kuhamia Yanga na klabu hiyo ina uhakika kwamba ishu itakwenda kirahisi kwani staa huyo ameshaanza 'kuingia kwenye mfumo'.
IHEFU
Inaweza kuwa ajabu lakini bado ni kwa asilimia ndogo. Wamiliki wapya wa Ihefu wanataka kumnasa mchezaji huyo kwa gharama yoyote wakiamini atawasaidia kurahisisha safari ya mafanikio.
Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka kwa watu wa karibu na Dube, mabosi wa Ihefu ambao zamani walikuwa wakiimiliki Klabu ya Singida United iliyopanda daraja mwaka 2017, walitaka kumsajili wakati ule sambamba na Tafadzwa Kutinyu.
Lakini Dube alichagua kwenda Afrika Kusini ambako hata hivyo hakufanikiwa na kuamua kurudi Zimbabwe.
Lakini sasa wakiwa na timu mpya, mabosi wale wamerejea tena kwa Prince Dube na kuivuruga akili yake kwa 'mzigo mrefu' waliomuwekea mezani. Lakini Yanga bado imemuingia akilini zaidi.
NYUMBANI ZIMBABWE
Habari kutoka Zimbabwe zinasema timu mbili nchini humo zinapigana vikumbo kumrudisha kijana wao.
Mwanaspoti linaijua Highlanders FC, timu aliyokulia Dube ambayo kwa sasa ina wamiliki wapya wenye 'mpunga mrefu' ambao wangependa kumrudisha nyota wao huyo kipenzi cha mashabiki wa timu.
Pia klabu ya Yadah FC ambayo hivi karibuni ilinasa saini ya nyota Khama Billiat nayo iko katika harakati za kumnasa Dube. Timu hizo mbili zinaitesa akili ya Dube, lakini Yanga wanazicheki tu.
Lakini taarifa nyingine zinasema Dube anaamini majeraha yanayomuandama pale Chamazi yanatokana na mambo ya nje ya uwanja hivyo anataka kuondoka ili kujiepusha nayo.
Mchezaji huyo alijiunga na Azam FC 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe - timu yake ya utotoni.
Aliyaanza maisha ya Chamazi kwa furaha kubwa kabla hajaumia kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Novemba 25, 2020 na tangu hapo hakurudi kuwa Dube wa kabla ya kuumia.
Msimu huu pekee ameshakosa mechi zaidi ya tano kutokana na majeraha ambayo hadi sasa yanamuweka nje.
Hata hivyo, kwa mujibu wa chanzo chetu ni kwamba kwa sasa hataki hata kurudi Chamazi akilazimisha kuondoka.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema Dube anatarajiwa kujiunga na timu hiyo wiki ijayo na kwamba, mchezaji huyo ana mkataba nao hadi mwaka 2026.
Hadi sasa Dube amecheza dakika 734 kati ya jumla ya dakika 1710 za mechi 19 za Azam FC msimu huu. Dakika hizo alizocheza ni katika mechi 12, huku akikosa mechi saba kati ya mechi 19 za msimu.
Kwa kifupi ni kwamba Dube amecheza chini ya nusu ya dakika za jumla kama angecheza mechi zote msimu huu na hii ni kutokana na pancha za hapa na pale ambazo kimsingi zimekuwa zikimuandama katika misimu yote.
Katika dakika hizo 734 za mechi 12 ambazo amecheza, amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao.
Mkataba wa Dube na Azam FC unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 2026, ikiwa na maana kwamba bado ana misimu miwili na nusu mbele.
ISHU KAMA YA FEI
Yanga inaonekana kujibu mashambulizi kama ambayo ilifanyiwa na Azam kumng'oa Feisal Salum ambaye alikuwa bado na mkataba Jangwani lakini timu hiyo ya matajiri wa jiji la Dar es Salaam ikamchukua baada ya mvutano mkali uliomalizwa na agizo la Rais wa Tanzania, Samia Hassan, aliyewataka Yanga wakamalizane naye ili kulinda kipaji chake.