Selembe kocha wa utimamu Mafunzo
Muktasari:
- Katika taarifa iliyotumwa na timu hiyo, ilisema Selembe anarejea Mafunzo katika eneo la benchi la ufundi baada ya hapo awali kuwa mchezaji wa kikosi hicho.
ALIYEKUWA nahodha wa timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Suleiman Kassim Suleiman ‘Selembe’ ametambulishwa na klabu ya Mafunzo kuwa kocha mpya wa utimamu wa mwili.
Katika taarifa iliyotumwa na timu hiyo, ilisema Selembe anarejea Mafunzo katika eneo la benchi la ufundi baada ya hapo awali kuwa mchezaji wa kikosi hicho.
“Tunamkaribisha rasmi Suleiman Kassim Suleiman kama kocha wetu mpya wa Utimamu wa Miili (Fitness Coach), uzalendo wake na uzoefu wake wa ndani ya uwanja ni chachu kubwa katika benchi letu la ufundi msimu huu,” ilisema taarifa hiyo
Wakati akiwa mchezaji akiitumikia Mafunzo kwa miaka 16, Selembe alikuwa sehemu ya wachezaji muhimu kiasi cha kuitwa mara kwa mara kuitumikia Zanzibar Heroes kwa mafanikio.
Timu nyingine alizowahi kucheza ni Malindi, Azam, JKT Tanzania, Costal Union, African Lyon, Polisi Tanzania, Stand United, Maji Maji na OC Bukavu Dawa ya DR Congo. Hatua ya utambulisho wa Selembe inakuja zikiwa zimepita wiki mbili tangu ahitimu kozi ya utimamu wa mwili Zanzibar.