Pondamali: Makipa wazawa wana kazi kubwa ya kufanya
ALIYEKUWA kocha wa makipa wa Yanga na Taifa Stars, Juma Pondamali, amesema, kuna kazi kubwa ya kufanya kwa wachezaji wazawa wanaocheza nafasi hiyo, kuhakikisha viwango vyao vinaendana na wageni.
Pondamali amesema ili makipa wawe wazuri, lazima misingi yao ianzie chini kwenye vituo vya soka, kuliko kuchukua ambao wamecheza ligi ya madaraja ya chini akibainisha kwamba wengi wao wametoka mitaani bila kupata misingi sahihi.
"Nafuatilia ligi, naangalia makosa mengi ya magolikipa, unaona misingi yao hawakupita katika vituo vya soka, hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya ili viwango vyao viweze kuendana na wageni," amesema.
Pondamanli amemtolea mfano kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra ambaye msimu uliopita alimaliza na cleansheets 18 za Ligi Kuu Bara akisema kwamba kiwango chake kinaonekana kimejengwa na misingi sahihi.
"Diarra alianza kucheza nafasi ya ndani, ndiyo maana ni rahisi wakati mwingine kuokoa hatari ama kuanzisha pasi kwa mguu akiwa anajiamini," amesema na kuongeza;
"Makipa wetu viwango vyao vikiendana na wageni litakuwa jambo jema, mfano hata kwenye cleansheets msimu huu wawe wageni, mwingine wazawa, hivi karibuni waliochukua ni Moussa Camara alikuwa na 19, akaja Diarra, natamani unaoisha tusikie Aishi Manula na wengine."