Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bayi: Michezo si kupoteza muda

BAYI Pict

Muktasari:

  • Pia wameshauri kuwepo kwa mashindano ya michezo ya shule kwa ngazi ya Afrika, akisema hatua hiyo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha kugundua na kuendeleza vipaji vya watoto baada ya kupitia kwenye mashindano ya shule za msingi na sekondari (Umitashumta na Umisseta) na yale ya Afrika Mashariki (Feassa).

WAKATI Tanzania ikijiandaa kushirikiana na Kenya na Uganda kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, wadau wa michezo wameitaka Serikali na shule nchini kuwekeza zaidi katika vipaji vya wanafunzi, wakisema michezo si burudani pekee bali ni njia ya kupata elimu, ajira na kujenga afya.

Pia wameshauri kuwepo kwa mashindano ya michezo ya shule kwa ngazi ya Afrika, akisema hatua hiyo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha kugundua na kuendeleza vipaji vya watoto baada ya kupitia kwenye mashindano ya shule za msingi na sekondari (Umitashumta na Umisseta) na yale ya Afrika Mashariki (Feassa).

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi za Filbert Bayi na mwanariadha nyota wa zamani, Filbert Bayi, amependekeza kuwepo kwa mashindano ya michezo ya shule kwa ngazi ya Afrika, akisema hatua hiyo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha kugundua na kuendeleza vipaji vya watoto.

Amesema Tanzania tayari ina mashindano ya shule za msingi na sekondari (Umitashumta na Umisseta) huku mashindano ya shule za Afrika Mashariki (Feassa) yakitoa msingi wa kupanua wigo ili kufikia ngazi ya kuwa na mashindano ya shule za Afrika akiamini ni fursa ya kujenga mfumo wa muda mrefu wa kugundua vipaji, kuviendeleza na kuvigeuza kuwa ajira na wataalamu wa michezo.

BAY 01

Bayi aligusia pia ushirikiano kati ya Serikali, shule, wazazi, vyama vya michezo na sekta binafsi kuwa chachu ya kumkuza  mtoto kitaaluma na michezo, akisisitiza kuwa michezo na taaluma haviwezi kutenganishwa na kuwashauri wazazi kuacha mtazamo kwamba mtoto anayeshiriki michezo anapoteza muda wa kusoma.

“Tunaposema nikicheza ni kupoteza muda, mimi siamini kabisa hiko kitu, sisi tulisoma mpaka vyuo vikuu tulikuwa tunacheza na tunasoma,” amesema na kuongeza kinachohitajika ni mwanafunzi kujifunza kupanga muda wake kati ya masomo na mazoezi, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mwanamichezo hayawezi kutegemea mwalimu au kocha pekee.

“Mwalimu atakupa njia tu, inabidi mchezaji mwenyewe iwe kwenye moyo wake, nia yake na kichwa chake yeye anataka awe mtu fulani na anataka ajiajiri kwenye mchezo huo,” amesema.

BAY 02

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Michezo, Sera na Utawala Bora, Godfrey Ng’umbi, amesema michezo inaweza kuwa daraja la mwanafunzi kupata elimu ya juu na fursa za ajira ndani na nje ya nchi, hivyo inapaswa kupewa nafasi sawa na taaluma darasani.

Ng’umbi, aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne wa Shule za Filbert Bayi, amesema, “Kwa mwanafunzi, michezo inakuza kipaji chake, inaboresha afya yake, lakini pia inampa nafasi kupitia kipaji chake kupata elimu na kusonga mbele,” amesema.

Alitoa mfano wa aliyekuwa mchezaji wa kikapu wa Tanzania, Hasheem Thabeet, ambaye alianza kucheza akiwa Tanzania kabla ya kipaji chake kumfikisha Marekani, akisema mifano hiyo inaonyesha namna michezo inaweza kubadilisha maisha ya vijana.

Ng’umbi pia alizitaka shule na Serikali kuangalia uwezekano wa kuimarisha akademi za michezo, hususan soka, ili kutumia maandalizi ya AFCON 2027 kama fursa ya kujenga kizazi cha wachezaji na wataalamu wa michezo watakaoiwakilisha Tanzania kwa muda mrefu.

BAY 03

Awali akieleza historia ya shule za Filbert Bayi, Mkurugenzi wa Taasisi za Filbert Bayi, Elizabeth Mjema, amesema shule hizo zenye kampasi tatu zinazotoa elimu ya awali na msingi Kimara na Mkuza Kibaha, pamoja na kampasi ya sekondari Kibaha zimeweka michezo kama sehemu ya maisha ya mwanafunzi, kwa kuwa inaamini inachangia afya, kujiamini na kuongeza hamasa ya kusoma.

Amesema wanafunzi hushiriki michezo kuanzia wanapoamka hadi wanapoingia darasani na baada ya masomo, akisema mfumo huo umesaidia kujenga wanafunzi wenye kujiamini na kuwa na nguvu za kushiriki shughuli za kielimu.

“Michezo ni furaha, michezo ni amani, lakini michezo inaongeza hamasa ya mwanafunzi kwenye kusoma,” amesema na kuongeza.

“Mfano shule yetu ya sekondari, imeendelea kupata ufaulu wa asilimia 100,  katika wanafunzi 53 waliomaliza kidato cha nne mwaka jana, 45 walipata nafasi za kuendelea kidato cha tano na wengine walipata nafasi katika vyuo mbalimbali, na wamekuwa wakishiriki michezo na taaluma vyema.”