KVZ yacheza dakika 450 bila ushindi
Muktasari:
- Katika dakika hizo 450 ilizocheza KVZ, imeambulia vipigo vinne ikianzia Kombe la Kagame ilipopoteza mechi tatu. Mechi nyingine ya kwanza ya ligi dhidi ya Polisi ikapoteza. Kabla ya hapo, ilimaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 dhidi ya KMKM katika Ngao ya Jamii, lakini ikaja kushinda kwa penalti 8-7.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ wameianza safari ya kutetea ubingwa wake na maandalizi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa namna ya kushangaza baada ya kucheza mechi tano sawa na dakika 450 bila ushindi wa kawaida.
Katika dakika hizo 450 ilizocheza KVZ, imeambulia vipigo vinne ikianzia Kombe la Kagame ilipopoteza mechi tatu. Mechi nyingine ya kwanza ya ligi dhidi ya Polisi ikapoteza. Kabla ya hapo, ilimaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 dhidi ya KMKM katika Ngao ya Jamii, lakini ikaja kushinda kwa penalti 8-7.
KVZ katika mechi tano, imefunga mabao mawili pekee, huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11. Matokeo ya mechi hizo yalikuwa kama ifuatavyo; Rayon Sports 2-0 KVZ, Al Hilal 4-0 KVZ, Tusker 2-0 KVZ, KMKM 2-2KVZ na Polisi 1-0 KVZ.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali, amesema sababu kuu ya kupoteza kwa michezo hiyo ni wachezaji kutokuwa makini uwanjani.
Alieleza kuwa, tatizo lingine ni mabeki wa pembeni wanaopaswa kuwavuta mawinga kwenye eneo la wapinzani wamekuwa hawasogei, ndio maana wanakaribisha sana mashambulizi.
Alipoulizwa kuhusu mtindo wake wa kubadilisha kikosi mara kwa mara huwa analenga nini, Hababuu amesema anafanya hivyo kutokana na kuwa na wachezaji wengi, hivyo anahitaji kuona kila mmoja atatoa kitu gani kipya kwa timu.
“Timu ina wachezaji wengi wapya, lengo ni kucheza na kuona kwamba tunapata kikosi ambacho kitaisaidia timu bila kutegemea mchezaji mmoja pekee,” amesema.
“Licha ya kupoteza mechi hizo, bado wana matumaini ya kufanya vizuri mbele ya safari kutokana na kupata ladha ya mechi za kimataifa kwenye mashindano ya Kagame.”
Ijumaa ya Septemba 4, 2026, KVZ itakuwa ugenini nchini Libya kuikabili Al Swehly SC katika mechi ya mkondo wa kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha timu hizo zitarudiana Septemba Septemba 13, 2026.