Polisi Tanzania wapata ajali, Mdamu avunjika miguu

KIKIOSI cha Polisi Tanzania kimepata ajali leo Ijumaa wakiwa wanatoka mazoezini katika Uwanja wa TPC wakielekea kambini.

Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Robert Munisi amesema; "Kwa sasa ni mapema kuwa na taarifa ya nini kilitokea lakini kwa kifupi gari liliacha njia na kugonga mti, hivyo kwa haraka walioumia ni zaidi ya wachezaji 10 na Mathias Mdamu amevunjika miguu yote miwili.

"Dereva wetu amevunjika mbavu moja, ndio taarifa za awali ninazoweza kukueleza lakini bado naendelea kufuatilia hapa KCMC walipokuwa majeruhi na kisha nitatoa majibu kamili ya kilichotokea," anasema Munisi.

Polisi Tanzania inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 42 na ilikuwa inajiandaa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliopangwa kuchezwa wiki ijayo katika Uwanja wa Ushirika Moshi.