Panga kubwa kupita Msimbazi, wanaoondoka, wanaobaki hawa hapa

Saturday May 14 2022
Sakho PIC
By Mwandishi Wetu

SIMBA haikuwa na mpango wa kufanya usajili mkubwa katiika dirisha kubwa lijalo la usajili baada ya kumalizika kwa msimu huu wa ligi lakini sababu mbalimbali hasa ufanisi wa nyota wake katika mechi za hivi karibuni hasa zile za kimataifa zimefanya ibadili gia angani.

Uongozi wa timu hiyo umepanga kupitisha panga kubwa katika kikosi chake cha sasa na kushusha vifaa vipya ambavyo vitaifanya iwe na makali maradufu msimu ujao baada ya kuwa na mwendo wa kusuasua msimu huu.

Kiwango kisichoridhisha cha baadhi ya nyota wake hasa wale wa kigeni kwenye michezo ya mashindano ya kimataifa hasa ile ya ugenini, kimeonekana kuwabadilisha mawazo vigogo wa Simba ambao wanaamini kuwa wangeweza kufika hatua ya nusu fainali au hata fainali ikiwa ingekuwa na wachezaji wa daraja la juu kuliko baadhi ilionao sasa.

Simba inaamini kwamba kama ingekuwa na kundi kubwa la wachezaji wa daraja la juu, isingeishia katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo walitolewa na Orlando Pirates kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Muda mfupi baada ya kutolewa na Orlando Pirates, kocha wa Simba, Pablo Franco alikiri hadharani kuwa timu yake inaangushwa na kiwango duni cha baadhi ya wachezaji wake katika michezo mikubwa.

‚ÄúImeonekana ni ngumu zaidi kwa Simba kupata matokeo mazuri katika michezo mikubwa kutokana na ubora ndani ya timu kuwa wa kawaida, tunahitaji kufanya vyema na ili iwe hivyo basi tunatakiwa kuwa na ongezeko la wachezaji bora ndani ya timu.”

Advertisement

“Ubora wa wachezaji ni muhimu kwa Simba na hatuwezi kuwa bora katika uongozi tukasahau ubora katika timu, lazima tuweke mipango ambayo itakuwa sahihi kwa afya ya timu yetu na bado tutaendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha tunafanikiwa katika mipango yetu,” alisema Pablo.

Kauli hiyo ya Pablo imeonekana kuufanya uongozi wa Simba kubadilisha lengo la awali na sasa utawafyeka wachezaji ambao viwango vyao vimeonekana havina msaada mkubwa kwa Simba huku wengine wakipewa mkono wa kwaheri kutokana na kutokuwa na mwenendo usioridhisha wa kinidhamu.

“Kuna wachezaji wataachwa kwa sababu ya utovu wa nidhamu. Timu imejaribu kuwapa nafasi kuona kama watajirekebisha lakini baadhi wanaonekana kutobadilika. Lakini pia tunahitaji watu wa maana ambao watatuvusha kimataifa kutoka robo fainali ambayo ni kama tumeshaizoea na kuingia nusu au fainali.”

“Angalia mchezaji kama Inonga (Henock) ameleta kitu cha tofauti kikosini kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akionyesha lakini anacheza kwa kujitolea akijua wajibu wake kwenye timu. Tunahitaji kuongeza wachezaji wa namna hiyo kwenye kikosi chetu na kuna sura zinaachwa hata mashabiki hawataamini,” kilisema chanzo cha kuaminika.

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti katika kikosi cha Simba imebaini majina ya wachezaji ambao wana nafasi kubwa ya kubaki, wale ambao kuna uwezekano wa kubaki au kuondoka na wale ambao watapewa mkono wa kwaheri.


AISHI MANULA - ANABAKI

Namna pekee ambayo Manula anaweza kuondoka Simba ni kuwepo kwa timu itakayompa kiasi kikubwa cha fedha ya nje au ndani ya nchi lakini bado yupo katika mipango ya timu hiyo na kila upande unaonyesha dalili za kuendelea kuwa na mwenzake.


BENO KAKOLANYA - ANABAKI

Licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, Simba bado inaonekana haina nia ya kumuachia Kakolanya aondoke kwa sasa ukizingatia ana mkataba wa mwaka mmoja amebakiza.


ALLY SALIM- 50/50

Upo uwezekano wa kuondoka lakini kama itaamriwa hivyo, atatolewa kwa mkopo kwa vile Simba inamtazama kama tegemezi la baadaye la timu hiyo.


SHOMARI KAPOMBE - ANABAKI

Bado ana mkataba wa kuitumikia Simba na bado ina mpango wa kuendelea naye kutokana na kiwango chake bora.


ISRAEL PATRICK - ANABAKI

Hapati nafasi ya kutosha mara kwa mara lakini Simba haina mpango wa kumuacha kwa sasa ikimtazama kama mrithi wa muda mrefu wa Kapombe.


MOHAMED HUSSEIN - ANABAKI

Uwezekano wa kuondoka Simba ni labda anunuliwe na timu itakayotoa ofa ambayo Simba watakubaliana nayo vinginevyo kiwango chake kinamlinda na ikumbukwe ni nahodha msaidizi.


GADIEL MICHAEL - 50/50

Ameonekana kushindwa kuhimili ushindani wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’. Simba inamsaka mchezaji mwingine wa ndani wa nafasi hiyo ambaye akipatikana, Gadiel ataachwa lakini kama akikosekana atabaki.


HENOCK INONGA - ANABAKI

Simba haina mpango wa kuachana naye kutokana na kiwango anachokionyesha


JOASH ONYANGO - ANABAKI

Simba inamshawishi abakie ingawa mkataba wake unalekea ukingoni hivyo ataondoka ikiwa watashindwa kufikia makubaliano.


PASCAL WAWA - ANAONDOKA

Simba itampa mkono wa kwaheri na nafasi yake itazibwa na beki wa kigeni ambaye atasajiliwa katika dirisha kubwa la usajili.


KENNEDY JUMA-ANABAKI

Hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara lakini Simba haina mpango wa kumuacha kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha kila anapopewa nafasi.


ERASTO NYONI - 50/50

Anaweza kuwacha au akabaki na hilo litategemea kama atapatikana au hatopatikana mchezaji mzawa ambaye kiwango chae kitaonekana bora kumzidi.


JONAS MKUDE - ANABAKI

Simba haina mpango wa kumuacha na bado ana mkataba wa kuitumikia timu hiyo.


TADDEO LWANGA - ANAONDOKA

Awali Simba haikuwa na mpango wa kumuacha lakini kiwango chake tangu alipopona majeraha na kurejea uwanjani kimeonekana kutowashawishi kubaki naye.


MZAMIRU YASSIN - ANABAKIA

Nidhamu na kujituma kwake ni mambo mawili ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kumuweka katika nafasi ya kubaki.


RALLY BWALYA - 50/50

Mkataba wake unaelekea ukingoni. Kama Simba itampata kiungo bora mpya kumzidi, hatoongezewa mkataba lakini ikiwa kinyume atabaki.


CLATOUS CHAMA - ANABAKI

Ndio kwanza ameanza kuutumikia mkataba wake wa miaka mitatu na Simba na haina mpango wa kuruhusu aondoke.


PAPE OSMANE SAKHO - 50/50

Kuna ofa mezani za kumhitaji kutoka klabu kadhaa ikiwemo Al Hilal ya Sudan. Akipatikana mchezaji anayeweza kuwa mbadala sahihi, kuna uwezekano mkubwa akauzwa lakini vinginevyo atabakia.


HASSAN DILUNGA-ANABAKI

Ataendelea kuitumikia Simba msimu ujao kwa vile bado yupo katika mipango yao.


PETER BANDA-50/50

Kama Simba itampata winga wa daraja la juu kumzidi, ataachwa kwa kutolewa kwa mkopo vingine tutamuona akiendelea kuvaa jezi yao msimu ujao.


BERNARD MORRISON - ANAONDOKA

Awali Simba iligawanyika ambapo wapo waliotaka abakia na wengine aondoke lakini mwenendo usioridhisha wa nidhamu yake, umeifanya iamue kutomuongezea mkataba mpya.


JOHN BOCCO - ANABAKI

Hajawa na msimu mzuri lakini Simba haina mpango wa kuachana naye kwa sasa kwa sababu ya nafasi yake kama nahodha.


JIMMYSON MWANUKE - 50/50

Anaweza kutolewa kwa mkopo ili kupata nafasi ya kutosha ya kucheza lakini Simba ina mipango naye ya muda mrefu.  


KIBU DENIS-ANABAKI

Timu hiyo haina mpango wa kuachana na Kibu Denis kwa sasa kutokana na kiwango anachokionyesha.


CHRIS MUGALU - ANAONDOKA

Hajafunga bao lolote kwenye Ligi Kuu ingawa amefumania nyavu mara mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika. Simba inasaka washambuliaji wapya kwa sasa na nyota huyo kutoka DR Congo atapewa mkono wa kwaheri.


MEDDIE KAGERE - ANAONDOKA

Ingawa rekodi yake katika kufumania nyavu ni nzuri tangu alipojiunga na Simba mwaka 2018, mshambuliaji huyo ataonyeshwa mlango wa kutokea kupisha ujio wa straika mpya.


SADIO KANOUTE - ANABAKI

Ameonyesha kiwango bora katika kikosi cha Simba na haina mpango wa kumuacha ukizingatia ana mkataba wa miaka mitatu wa kuitumikia timu hiyo.


YUSUPH MHILU - 50/50

Kama Simba ikipata mchezaji mzawa wa nafasi yake ambaye ana ubora kumzidi, Mhilu ataachwa na Simba ila vinginevyo atabakia.


WADAU WAFUNGUKA

Kocha na nyota wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden alisema kuwa usajili wa nyota wapya hauepukiki katika timu hiyo msimu ujao.

“Simba haina kikosi kibaya ila kinapaswa kuongezewa nguvu kwa kuongezewa baadhi ya wachezaji ili timu iwe imara zaidi. Nafasi za kuimarisha ni mshambuliaji wa kati, kiungo na hata beki wa kati,” alisema Kibaden.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kuwa kama Simba ina mpango wa kufanya vizuri kimataifa, inapaswa kusajili wachezaji wanaofahamu vyema mashindano hayo.

“Simba walijiwekea malengo yao kwenye mechi za kimataifa ambayo yalikuwa ni kutinga nusu fainali au fainali. Kama wana hayo malengo ni lazima wabadilishe kikosi. Waqchezaji walionao wengi hawana uzoefu wa hatua hizo kubwa. Maingizo yao mapya yaliangalia kufanya biashara. Lakini kwa sasa haijafanikiwa na kama inataka yaje kutimia hakuna namna ni lazima ifanye usajili. Nafasi inazotakiwa kusajili ni upande wa beki wa kushoto. beki mmoja wa kimataifa mwepesi, mwenye spidi anayeweza kuruka vichwa.”

“Wanahitaji kiungo mkabaji ili mpira usifike katika mstari wa walinzi lakini pia wanahitaji washambuliaji wa daraja la juu ama wawili au mmoja ambao wanaweza kuipa timu matokeo mazuri hasa pale ikikutana na wapinzani walio bora,” alisema Pawasa.


Advertisement