Manqoba Mngqithi atuma ujumbe mzito Yanga ikichapwa na Wakongo
Muktasari:
- Mngqithi amesema mchezo huo wa kirafiki uliochezwa leo Jumapili Agosti 9, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, umeonyesha mambo kadhaa yanayohitaji kurekebishwa, lakini pia umeibua matumaini makubwa kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na baadhi ya wachezaji, hasa vijana.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema licha ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Les Aigles Du Congo katika tamasha la Yanga Day, lakini anaamini kikosi chake kina uwezo wa kufanya vizuri msimu ujao, ikiwamo kushindana kwa nguvu katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mngqithi amesema mchezo huo wa kirafiki uliochezwa leo Jumapili Agosti 9, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, umeonyesha mambo kadhaa yanayohitaji kurekebishwa, lakini pia umeibua matumaini makubwa kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na baadhi ya wachezaji, hasa vijana.
Yanga ilianza kufunga dakika 27 kupitia Peter Shalulile kwa mkwaju wa penalti, kisha Wakongomani wakasawazisha dakika ya 36 na 65, mabao yote yakifungwa na Tonny Talasi.
Akizungumzia bao la kwanza walilofungwa, kocha huyo amesema lilitokana na makosa ya kizembe ambayo timu inapaswa kuyafanyia kazi kabla ya msimu kuanza.
“Ulikuwa mpira mrefu ambao kwa bahati mbaya Okello (Allan) alikuwa katika muda wa kuupokea, lakini mchezaji mwenzake alimvuruga. Hiyo ikawa nafasi kwa wapinzani. Kwa kweli, lilikuwa bao la kijinga sana,” amesema.
Amesema kipindi cha pili timu ilionyesha mwitikio mzuri na kutengeneza nafasi kadhaa katika eneo la mwisho, lakini tatizo lilikuwa kushindwa kuzitumia.
“Tulianza kipindi cha pili vizuri. Ilionekana kama tungeweza kufunga wakati wowote. Tulitengeneza nyakati nzuri katika eneo la mwisho, lakini kwa bahati mbaya hatukutumia nafasi zetu,” amesema mkufunzi huyo kutoka Afrika Kusini.
Kocha huyo ameongeza kuwa, baadhi ya makosa katika eneo la mwisho yaliipa timu pinzani nafasi ya kupata bao la pili.
“Tumefanya makosa ya kijinga katika eneo la mwisho. Wao walipata nafasi moja nzuri na wakaitumia. Ilitokana na mchezaji kijana ambaye hakuwa katika nafasi sahihi na tukapata adhabu.”
Kocha huyo amesema mchezo unaofuata Jumatano dhidi ya Simba katika Ngao ya Jamii, utakuwa na sura tofauti, akieleza kuwa kikosi cha kwanza kinatarajiwa kupewa nafasi zaidi baada ya benchi la ufundi kufanya mchanganyiko wa wachezaji walipokabiliana na Les Aigles Du Congo.
“Nimefurahishwa na vijana waliopewa nafasi, lakini Jumatano itakuwa biashara halisi kwa kikosi cha kwanza kuonyesha kile wanachoweza kutupa,” amesema.
Amesema mpango wa kubadilisha kikosi ulilenga kuhakikisha wachezaji wanapata muda wa kucheza huku timu ikiendelea kujenga mwendelezo kuelekea msimu mpya.
“Tulipaswa kusawazisha vikosi viwili na kuhakikisha tunakuwa na mwendelezo. Nimeona mambo mengi mazuri ya kiuchezaji kutoka kwa timu na hilo ni jambo zuri.”
Pamoja na changamoto hizo, kocha huyo amewataka mashabiki kuwa na subira, akiahidi kuwa Yanga itakuwa na kikosi chenye nguvu msimu huu.
“Timu yetu ni imara. Ninaweza kuwaahidi mashabiki kwamba tutakuwa na timu yenye nguvu sana, ambayo inaweza kwenda mbali hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo yatahitaji muda na kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika maandalizi.
“Tunapaswa kuwa na subira. Makosa mengi tuliyofanya yametokana na wachezaji vijana, lakini hata wachezaji wakubwa wanapaswa kuonyesha uwezo wao,” amesema.
Kocha huyo pia alikosoa safu ya ulinzi kwa kupoteza mipira katika mazingira ambayo haikuwa chini ya presha.
“Nadhani safu ya mwisho ya ulinzi ilipoteza mipira mingi bila hata kuwa chini ya presha. Tukirekebisha hayo machache, tutakuwa na timu yenye ushindani mkubwa msimu huu.”
Akizungumzia tamasha la Yanga Day, kocha huyo amewashukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi na kuipa timu hamasa, akisema uwepo wao ni sehemu muhimu ya safari ya msimu mpya.
“Lilikuwa tukio la kuvutia sana. Tunawashukuru Wananchi kwa kutupa mazingira mazuri. Pia tunapaswa kuwaomba radhi kwa kutowapa matokeo baada ya wao kujitokeza kwa wingi,” amesema.
Amesema mashabiki hawakukata tamaa licha ya timu kupitia nyakati ngumu ndani ya mchezo.
“Walikuwa nasi muda wote wa mchezo. Katika nyakati ngumu walikuwepo na katika nyakati nzuri pia walikuwepo. Ninaweza kuwaahidi kwamba tuko kwenye mpango mzuri sana msimu huu,” amesema.
Kocha huyo ametoa ujumbe wa mwisho kwa mashabiki, akiwataka kuendelea kujitokeza kwa wingi katika michezo ya nyumbani.
“Endeleeni kuja kwa wingi. Tunathamini sana sapoti yenu. Mchezaji wa 12 atakuwa na maana kubwa sana kwetu. Ninaweza kuwaahidi kwamba mtapenda kile mtakachokiona msimu huu,” amesema.
Baada ya kumaliza tamasha la Yanga Day, Agosti 12, 2026, Yanga itacheza dhidi ya Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 2:30 usiku.