Pandu apongeza maendeleo ya michezo
Muktasari:
- Amewataka, wachezaji wa netiboli kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, nidhamu na kujitolea ili kufikia viwango vya juu kupata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kimataifa.
NAIBU Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Seif Kombo Pandu amesema maendeleo ya michezo kisiwani hapa yanaonyesha dhamira ya wananchi na viongozi katika kuendeleza vipaji, kuimarisha umoja na kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Ligi Kuu Netiboli Zanzibar iliyofanyika Uwanja wa Gymkanah, Pandu amesema hatua hiyo ni uthibitisho uwekezaji katika michezo unaendelea kuzaa matunda na unapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kuendeleza vipaji hivyo.
Amesema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kuimarisha ushindani na kuwakutanisha wananchi katika mazingira ya mshikamano.
“Michezo ni nyenzo ya kujenga umoja na afya kwa jamii, sambamba na kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi ambao wamekuwa wakihimiza wananchi kushiriki shughuli za michezo kwa manufaa ya maendeleo ya taifa,” amesema.
Aidha, amesema sekta ya michezo ni chanzo kikubwa cha ajira huku akibainisha wanamichezo wengi kwa sasa wanapata mapato kupitia vipaji vyao, hivyo vijana wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa kuongeza bidii na kujituma kwenye mashindano ambayo yanaandaliwa.
Amewataka, wachezaji wa netiboli kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, nidhamu na kujitolea ili kufikia viwango vya juu kupata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kimataifa.
Vilevile, amesisitiza maendeleo ya michezo yanahitaji ushirikiano wa viongozi, waandaaji, wadhamini na jamii kwa jumla ili kuhakikisha vipaji vinaendelezwa na michezo inakuwa nguzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.