Uhamiaji upepo umebadilika Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Uhamiaji itashuka dimbani Oktoba 29, 2026 ikikaribishwa na KMKM kwenye uwanja wa Mao B, uliopo Unguja.
BAADA ya Uhamiaji kufanya vizuri kwenye mechi tano za Ligi Kuu Zanzibar, upepo umebadilika upande wao wajikuta wakipoteza mechi tatu mfululizo kwenye ligi hiyo.
JKU ilikuwa timu ya mwanzo kuvuruga mipango ya timu hiyo kwa kuifunga mabao 3-1 kisha Mafunzo ikapata ushindi wa kwanza wa ligi kwa ushindi wa bao 1-0 na Polisi iliwatembezea kipigo cha mabao 3-1.
Akizungumza na Mwanaspoti Ofisa Habari na Msemaji wa timu hiyo, Mwinyi Hamad amesema hizo ni miongoni mwa changamoto za mpira hivyo watajitahidi kurekebisha makosa.
Amesema, licha ya hivyo matokeo ni juhudi, upande wao wanaedelea kuzifanya ijapokuwa haijawa bahati na hawastahili kuvunjika moyo kwa kuwa wapo kwenye hali nzuri ya msimamo wa ligi.
"Bado tuna nafasi ya kurekebisha makosa yanayojitokeza uwanjani hivyo siyo wakati wa kuikatia tamaa timu ambayo inamweleko mzuri," amesema
Mwinyi alisisitiza timu ipo vizuri kwa sababu haijapoteza mwelekeo na wachezaji wataendelea kuipambani Uhamiaji na kupoteza mechi tatu mfululizo isiwe sababu ya mashabiki wa timu hiyo kuacha kufika uwanjani kuwapa hamasa wachezaji.
Msemaji huyo, amesema kupoteza kwao kunawafanya kuongeza kasi ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zao ili wafanye vizuri michezo ijayo.
Uhamiaji itashuka dimbani Oktoba 29, 2026 ikikaribishwa na KMKM kwenye uwanja wa Mao B, uliopo Unguja.