Nyota wanne watemwa Simba, Morrison awahishwa hospitali
KIKOSI cha Simba kimeondoka nchini asubuhi ya leo Ijumaa Desemba 18 na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuelekea jijini Harare, Zimbabwe na watakaa kambi hapo kwa siku tano kabla ya kucheza na FC Platinum.
Simba watacheza mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa Desemba 23 mwaka huu.
Simba chini ya kocha mkuu Sven Vandenbroeck wameondoka na wachezaji 24, akiwemo nyota mpya aliyesajiliwa dirisha dogo Mganda Taddeo Lwanga huku wengine wanne wakibaki nchini kwa sababu mbalimbali ikiwemo Bernard Morrison.
Meneja wa Simba, Abass Selemani amesema wachezaji waliobaki ni Morrison ambaye anaumwa na alishindwa kufanya mazoezi na wenzake na leo Ijumaa atapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi.
Abbas amesema wachezaji wengine waliobaki ni David Kameta ambaye amechelewa kuomba kibali cha safari kwani alikuwa na timu ya taifa ya vijana, Kennedy Juma na Charles Ilanfya.
"Ukaichana na wachezaji hao wengine wote tunaondoka nao ili ikitokea kama tumeenda kufanya vipimo vya virusi vya corona na wakataka kutufanyia vigisu kwa baadhi ya wachezaji wetu kama ilivyokuwa Nigeria tusiwe na wasiwasi wowote,
"Wachezaji wote wapo na morali ya hali ya juu kushindana katika mechi hiyo, ili kupata matokeo mazuri ingawa tunatambua haitakuwa kazi rahisi kwani wote ambao tunakutana ni mabingwa wa nchi zao.
"Tunatambua mahala ambapo tunafikia kwani tayari kuna watu wetu wametangulia kuweka mazingira sawa na tuna imani kubwa kila kitu ambacho tutakwenda kukitumia huko kitakuwa katika mazingira salama na sahihi kwa mahitaji ya timu yetu," amesema Abbas