Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Simba ina nafasi ya kufuzu Caf’

Muktasari:

Simba inaondoka nchini leo kwenda Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platnum.

Dar es Salaam. Dakika 90 za mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya mabingwa watetezi Simba dhidi ya KMC zilimalizika kwa utata wa mkwaju wa penalti uliowapa Simba ushindi.

Penalti iliyozua utata ilitokea dakika ya 74, wakati mwamuzi Elly Sasii wa Dar es Salaam alipoamuru pigo hilo akidhani winga Salum Kabunda aliunawa mpira wakati akitaka kuokoa akiwa na beki Israel Mwenda.

Hata hivyo, picha za marudio ya video zilimhukumu Sasii na kuonekana hakuliona vyema tukio hilo na kuwapa uhalali KMC ambao walionekana kulalamikia takribani dakika moja uamuzi huo wakigomea kwamba haikuwa penalti.

Ndani ya dakika 90 KMC walionekana kufanikiwa kuibana vyema Simba na kuziba njia zao za kumalizia vyema mashambulizi yao wakiwa na nidhamu bora ya ukabaji.

Walichofanya ni kwamba walitangulia kuiheshimu Simba na kuwabana vyema kuanzia katikati mpaka katika safu yao ya ulinzi wakiwa na ubora mkubwa wa kukaba lakini pia kupunguza makosa.

Walijua Simba kama ni mashambulizi ya katikati mtu hatari kwao ni Clatous Chama, ambaye walifanikiwa kumpa ulinzi mzuri kwa kuzima pasi zake za hatari, huku Luis Miquissone naye wakimtuliza.

Simba kwa mara nyingine walionekana kupata wakati mgumu kwa kukosa mbinu mbadala, KMC walionekana kuibana vizuri baada ya kujua ubora wao na hakukuwa na mbadala wa mbinu kwa wekundu hao.

Kiungo mkongwe wa KMC Mugiraneza Jean, ambaye alionekana kulalamikia uamuzi wa mwamuzi, alisema Sasii aliharibu mchezo huo huku kocha wake akionekana kutotaka kuzungumzia hilo.

Mugiraneza alisema katika kuongea na Sasii alikuwa anamuomba akaombe kuangalia hata marudio ya video katika moja ya camera iliyokuwa nyuma ya lango lao kwa kuwa hakuna ambaye alikaribia hata kuugusa mpira kwa mkono.

“Mwamuzi (Sasii) alikosea sana, aliharibu hii mechi amewatengenezea ushindi Simba ,haikuwa penalti kabisa aliamua kwa kusikiliza kelele za mashabiki,” alisema Mugiraneza raia wa Rwanda.

Lakini kubwa lilikuwa kiwango cha Simba, ambacho kilionekana kuwapa matokeo kwa jasho tofauti na jinsi ilivyozoeleka kwa mashabiki wake tangu mwanzo wa ligi.

Simba ilianza kuwa taratibu uwanjani katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania, ambao uliwalazimu Chama na Bocco kuingia kuipa Simba mabao mawili yaliyofungwa na kiungo huyo wa Zambia.

Lakini pia, ilisota kupata matokeo katika mchezo dhidi ya vibonde, Mbeya City, wakilazimika kushinda kwa bao 1-0, kabla ya mchezo wa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa kushinda kwa penalti ya utata.

Akizungumzia mwenendo wa mabingwa hao na safari yao ya leo kwenda Zimbabwe kuikabili Platnum kwenye mzungo wa awali wa kusaka nafasi ya makundi, kocha wa Biashara United, anaamini Simba ina uwezo bado wa kupata matokeo ugenini.

“Ninachoona mimi Simba wanacheza vizuri.Wanacheza kama timu kwa ushirikiano, licha ya kwamba hawapati mabao mengi hilo haliifanyi timu hiyo kuonekana kama imeshuka kiwango.

“Tangu mechi yao iliyopita ya kimataifa dhidi ya Plateau United na hata waliporejea kwenye ligi hawajaruhusu bao sasa unaona ni jinsi gani wako vizuri,” alisema Baraza.

Kocha Mohammed Adolph Rishard alisema bado Simba wana nafasi ya kutisha kwenye mashindano ya kimataifa licha ya kwamba wameonekana kama hawakucheza vizuri katika mechi zao mbili zilizopita.

“Ujue kupata mabao mengi au machache ni jinsi mpinzani wako alivyo uwanjani. Hivyo hata Simba inategemea siku hiyo wamekutana na nani, si kila mara watashinda tu idadi kubwa ya mabao kama watu walivyowazoea.

“Bado wanacheza vizuri na wanaweza wakashangaza kwenye mashindano ya kimataifa muhimu ni kuhakikisha mechi hiyo ya ugenini wanacheza kwa nidhamu na kuhakikisha hata wanapata mabao ili iwe kazi rahisi watakapokuwa nyumbani kwenye mechi ya marudiano, “ alisema Rishard.