Nickson Kibabage aipa pigo Simba
Muktasari:
- Kukosekana kwa Kibabage kipindi hicho, ni pigo kwa Simba ambayo pia inamkosa Antony Mligo anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mechi dhidi ya Singida Black Stars, hivyo anatarajiwa kukosekana mechi tatu za Ligi Kuu Bara.
KIKOSI cha Simba kilikuwa na mechi ya Ligi Kuu Bara jana dhidi ya Coastal Union, ila habari mbaya kwa mashabiki wa timu hiyo ni baada ya kugundulika beki wa kushoto, Nickson Kibabage atakosekana uwanjani kwa zaidi ya wiki tatu hadi nne.
Kukosekana kwa Kibabage kipindi hicho, ni pigo kwa Simba ambayo pia inamkosa Antony Mligo anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mechi dhidi ya Singida Black Stars, hivyo anatarajiwa kukosekana mechi tatu za Ligi Kuu Bara.
Kibabage alipata majeraha hayo katika mechi ya kwanza ya msimu wa 2026-2027 ya Ligi Kuu Bara, ambayo Simba ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, kwenye Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera, Agosti 16, 2026.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kwamba beki huyo amepata majeraha hayo ya misuli ya paja (hamstring) na anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu hadi nne, kwa ajili ya kujiuguza vizuri kabla ya kurejea.
Chanzo hicho kilisema licha ya majeraha hayo kutoonekana siriazi zaidi, ila amegundulika atakosekana kwa kipindi hicho, ndio maana alikosekana kwa mechi tatu mfululizo ambazo ni dhidi ya Pamba Jiji, Singida Black Stars na Coastal Union.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na waandishi wa habari, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wachezaji wote wanaendelea vizuri wakiwemo pia kipa, Mahamadou Tanja Kassali na kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma.
“Kibabage anaendelea vizuri na kuanzia tarehe 25 au 26, tutakuwa na taarifa sahihi, kwa Kagoma alipata changamoto kabla ya mechi yetu na Singida, ila madaktari walimtaka apumzike ili apate muda mzuri wa kucheza mechi zijazo,” amesema Ally.
Aidha, Ally amesema kwa upande wa kipa wa kikosi hicho, Mahamadou Tanja Kassali aliyeumia katika mechi dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 16, 2026, anaendelea vizuri na matibabu yake ni ya kutumia dawa na sio suala la yeye kufanyiwa upasuaji.
Kibabage aliyejiunga na Simba, Januari 19, 2026, akitokea Singida Black Stars, ni miongoni mwa mabeki bora wa kushoto wa timu hiyo kwa sasa, kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha, licha ya uwepo wa nyota mwenzake, Anthony Mligo.
Hata hivyo, baada ya Mligo kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars, Agosti 22, 2026, imezidi kuongeza upungufu wa eneo hilo.
Mligo aliyeanza kutumikia adhabu hiyo katika mechi ya jana dhidi ya Coastal Union, itamfanya Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker kuamua kumtumia beki wa kulia, Nathaniel Chilambo ambaye ana uwezo mkubwa wa kucheza kushoto tangu akiwa Azam FC.