Prime
Vurugu zinavyotishia usalama wa soka Zanzibar – sehemu ya pili
Usalama wa uwanja wa mpira hauishii katika kuhakikisha mashabiki wanaingia kwa tiketi na mchezo unaanza kwa wakati.
Chini ya sheria, kanuni na miongozo ya usalama wa michezo, waandaaji wa mashindano, wasimamizi wa viwanja na mamlaka za soka wana wajibu wa kuweka mazingira yanayolinda wachezaji, waamuzi, viongozi, mashabiki na watu wengine wanaohusika katika mchezo.
Hata hivyo, matukio ya vurugu yaliyojitokeza katika baadhi ya viwanja Zanzibar yanaibua swali kuhusu namna matakwa hayo yanavyotekelezwa katika mazingira halisi.
Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya mashabiki kuvamia eneo la mchezo, waamuzi kuhitaji ulinzi baada ya mechi na vurugu kusababisha michezo kusimama au kuvunjika.
Lakini nyuma ya matukio hayo kuna mfumo wa sheria, kanuni na miongozo unaoweka wazi wajibu wa kuzuia hali hizo.
Kanuni zinasemaje?
Kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) za Usalama na Ulinzi, usalama wa uwanja unapaswa kupangwa kabla na wakati wa mchezo ili kuhakikisha watu walio katika uwanja wanalindwa. Miongoni mwa maeneo yanayopewa uzito ni eneo ambalo mchezo unafanyika.
Ibara ya 38 ya kanuni hizo inaweka matakwa ya kulinda eneo hilo dhidi ya uvamizi wa watazamaji. Kanuni zinaweka uwepo wa mfumo wa usalama, ukiwamo matumizi ya walinzi au usanifu wa uwanja unaozuia watazamaji kuingia kirahisi kwenye eneo la mchezo.
Vilevile, Kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) za Usalama na Ulinzi zinaweka wajibu kwa wasimamizi wa uwanja.
Ibara ya 16(i) ya kanuni hizo inaelekeza kwenye wajibu wa kuwalinda waamuzi na wachezaji wanapoingia uwanjani, wanapokuwa katika eneo la mchezo na wanapotoka.
Mbali na ulinzi wa watu, kanuni za FIFA zinaweka matakwa kuhusu muundo wa uwanja.
Ibara ya 31 inaelekeza kuwepo kwa ukuta au uzio wenye urefu usiopungua mita 2.5 kwa lengo la kuzuia watu wasiohusika kuingia eneo la mchezo.
Kanuni hizo za usalama hazitoi wajibu pekee, bali ukiukaji unaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 66 ya Kanuni za FIFA, ukiukaji wa masharti unaweza kusababisha hatua za kinidhamu chini ya Kanuni za Nidhamu za FIFA, zikiwamo faini, kufungiwa kwa viwanja au michezo kuchezwa bila mashabiki.
Kwa upande wa Zanzibar, Bodi ya Ligi (ZBL) ina mfumo wa adhabu ndani ya kanuni zake za mashindano.
Mtendaji Mkuu wa ZBL, Issa Kassim Ali, anasema Kanuni ya 3 ya Mashindano ya msimu wa 2024/25 inaweka adhabu kwa mtu anayemzuia mwamuzi kutekeleza majukumu yake.
Kanuni hiyo inasema: “Kumzuia mwamuzi kufanya kazi yake ni kosa na adhabu yake ni kumfungia aliyetenda kosa hilo awe shabiki, kiongozi au mtu yeyote kufika uwanjani kwa muda maalumu na kutozwa faini isiyopungua Sh500,000.”
Anasema iwapo shabiki aliyefanya vurugu hatatambulika, klabu yake inaweza kubeba adhabu hiyo.
Hivyo, mfumo wa ndani unaweka uwajibikaji wa mtu binafsi na wa klabu, huku kanuni za kimataifa zikiweka wajibu mpana zaidi kuhusu usalama wa tukio na miundombinu.
Usimamizi wa michezo pia una msingi wa kisheria kupitia Sheria ya Baraza la Michezo Zanzibar ya Mwaka 2010.
Kifungu cha 6(b) kinahusisha wajibu wa Baraza la Michezo kuhakikisha kiwango cha juu cha uanamichezo na nidhamu kwa wanamichezo na viongozi wote. Pia kifungu cha 6 (d) kinatoa mamlaka kwa Baraza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtu yeyote, klabu au kikundi cha mashabiki kinachovunja kanuni zilizowekwa.
Si hivyo tu, Sera ya Michezo ya Zanzibar ya Mwaka 2018, chini ya kaulimbiu ya “Michezo kwa Wote,” inasisitiza ujenzi wa mazingira jumuishi na salama ya michezo.
Kwa mtazamo huo, usalama haupaswi kuchukuliwa kama hatua inayochukuliwa baada ya vurugu kutokea. Unapaswa kuwa sehemu ya mazingira ya mchezo tangu uwanja unapopangwa, mashabiki wanapoingia, timu zinapowasili, mchezo unapoanza hadi watu wote wanapoondoka.
Mbali ya kanuni na sheria, mwaka 2024, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela) kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo Serikali, kiliandaa mwongozo wa kulinda usalama na ustawi katika michezo Zanzibar.
Mwongozo huo unalenga kuweka mfumo wa namna ya kuzuia na kushughulikia vitendo vya unyanyasaji, unyonyaji, ubaguzi, ukatili na aina nyingine za madhara dhidi ya washiriki wa michezo, hususani watoto na watu walio katika mazingira hatarishi.
Nani anawajibika?
Mchanganyiko wa sheria na kanuni hizo unaonyesha kuwa jukumu la usalama haliko kwa muhusika mmoja. Klabu ina wajibu wa kuwajibisha wachezaji, viongozi na mashabiki wake.
Mratibu wa mechi ana wajibu wa kupanga usalama wa mchezo, wasimamizi wa uwanja wana wajibu wa kuhakikisha miundombinu na mifumo ya usalama inafanya kazi. Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) na Bodi ya Ligi (ZBL) zina wajibu wa kusimamia mashindano na kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji, huku Serikali nayo ina wajibu katika eneo la miundombinu, sera na usimamizi wa sekta ya michezo.
Mtazamo wa wadau
Mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya soka Zanzibar, Abdulrahman Sadick Mussa, anasema uwepo wa sheria na kanuni pekee hautoshi bila utekelezaji.
“Sheria na kanuni zinapoweka wajibu wa kuhakikisha usalama, wajibu huo haupaswi kubaki kwenye karatasi. Kila anayehusika na mchezo anatakiwa kujua jukumu lake na pale linaposhindikana, kuwe na utaratibu wa kuhoji,” anasema na kuongeza:
“Kama shabiki amefanya kosa, awajibishwe. Kama klabu imehusika au imeshindwa kuchukua hatua zinazotakiwa nayo iwajibike. Kama tatizo ni uwanja kutokidhi viwango vya usalama, mwenye jukumu la kuhakikisha viwango hivyo vinatimizwa naye hawezi kukwepa kuwajibika.”
“Adhabu ni hatua baada ya kosa, lakini mfumo mzuri wa usalama unatakiwa kuzuia kosa lisitokee. Kwa hiyo, tunapaswa kujiuliza si tu nani amepigwa faini, bali ni kwa nini tukio limetokea na ni mfumo gani ulioshindwa kulizuia,” anasema.
Abdulrahman anasema: “Tusisubiri mwamuzi apigwe, mchezaji avamiwe au mchezo uvunjike ndipo tuanze kutafuta nani anawajibika. Usalama unatakiwa kupangwa kabla ya tukio. Tukifanya hivyo, tutakuwa tunalinda si mchezo pekee, bali pia heshima ya soka la Zanzibar.”
Kocha wa klabu ya Chipukizi inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, Suleiman Mohammed ‘Gamera’, anasema usalama wa wachezaji na waamuzi unapaswa kupewa kipaumbele sawa na maandalizi ya kiufundi.
“Kabla ya kocha kuangalia mfumo wa 4-3-3 au 4-4-2, waandaaji wanapaswa kujua kama mazingira ya mchezo ni salama. Mchezaji hawezi kucheza kwa utulivu kama anaona mashabiki wanaweza kuingia uwanjani wakati wowote,” anasema.
Anasema kutokuwapo kwa miundombinu mizuri katika baadhi ya viwanja kunaongeza changamoto.
“Uzio ni muhimu, lakini si uzio pekee. Tunahitaji milango inayodhibitiwa, njia maalumu za waamuzi na wachezaji, walinzi wa kutosha na mpango wa dharura. Hapo ndipo utaweza kusema mchezo umeandaliwa kitaalamu,” anasema.
Nyota wa zamani wa Miembeni FC, Mzee Maneno, anasema usalama wa viwanja Zanzibar unahitaji kuangaliwa kwa upana akieleza kuwa, vurugu zinapojitokeza haziathiri mchezo pekee, bali pia taswira ya soka la Zanzibar.
“Usalama wa mchezo unatakiwa kuanza kabla ya mpira kuchezwa. Kama tunajua kuna mechi yenye presha kubwa, lazima maandalizi ya usalama yawe makubwa. Huwezi kuwa na mashabiki wengi halafu walinzi ni wachache na kutegemea kila kitu kitakwenda vizuri.”
Anasema waamuzi wanahitaji kulindwa kwa sababu uamuzi wao ni sehemu ya mchezo na kutoridhika na uamuzi hakumpi mtu haki ya kumshambulia mwamuzi.
“Mwamuzi akifanya kosa, kanuni zipo za kumchukulia hatua, lakini si sahihi mchezaji, kiongozi au shabiki kumvamia. Tukiruhusu jambo hili tutafika mahali waamuzi wataogopa kuchezesha mechi na soka litapoteza maana yake,”.
Naye, Mgeni Sudi ‘Bingwa’, anayeshabikia timu ya Miembeni FC, anasema klabu zina jukumu kubwa la kuelimisha mashabiki wao kuhusu nidhamu na iwapo kuna tatizo njia rasmi zitumike kuwasilisha malalamiko.
Kwa upande wake, Joseph John, anasema uwajibikaji haupaswi kuishia kwa shabiki anayefanya vurugu, bali kuangalia maandalizi ya uwanja, ulinzi na iwapo kuna uzembe, wahusika wawajibishwe.