Prime
Kocha Simba atishia rekodi Yanga
TANGU Desemba 19, 2026 Simba ilipomtambulisha Steve Barker kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Msauzi huyo amekuwa na mwendo mzuri wa kuiongoza timu hiyo inayopambana kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara ilioukosa misimu mitano mfululizo.
Wakati Simba inateseka ikiusaka ubingwa wa ligi ilioushinda mara ya mwisho msimu wa 2020-2021, Yanga inaendelea kutamba ikibeba 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026.
Barker anaonekana kama kuna kitu amekibadilisha ndani ya Simba na huenda akaipa timu hiyo taji la Ligi Kuu Bara endapo atafanikiwa kumaliza msimu huu kwani suala la makocha kusitishiwa mikataba limekuwa sio la kutabirika.
Kocha huyo kabla ya jana kuiongoza Simba kucheza dhidi ya Coastal Union, amefanikiwa kuisimamia katika mechi 28 za Ligi Kuu Bara akiwa hajapoteza hata moja. Mechi hizo 28 ni sawa na dakika 2,520 ambapo Barker ameonesha ubabe wake huku akitishia rekodi ya Yanga ambayo ilicheza michezo 49 bila kupoteza.
Katika mechi hizo, Simba imeshinda 21 na sare saba, huku ikikusanya jumla ya pointi 70 kati ya 84 zilizokuwa kwenye michezo hiyo.
Rekodi hiyo inaonyesha kiwango cha juu cha ushindani cha timu hiyo, ambayo imekuwa na uwezo wa kupata matokeo chanya dhidi ya wapinzani mbalimbali, ikiwemo Yanga, Azam FC, Singida BS, Pamba Jiji, Mtibwa Sugar na Coastal Union.
MABAO 49
Katika mechi hizo 28, Simba imefunga jumla ya mabao 49, ikiwa na wastani wa bao 1.75 kwa kila mchezo.
Ushindi mkubwa zaidi katika kipindi hicho ulikuwa wa 4-0 dhidi ya TZ Prisons, huku pia ikipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United, Fountain Gate, Namungo FC, Mashujaa FC na Mtibwa Sugar.
Kwa upande mwingine, Simba imefungwa mabao 10 pekee, ikiwa na wastani wa 0.36 kwa kila mchezo. Hii inaifanya timu hiyo kuwa na tofauti ya mabao +39, ishara ya ubora katika safu zote mbili.
Simba pia imefanikiwa kumaliza mechi bila ya kuruhusu bao ‘clean sheet’ mara 19, sawa na asilimia 67.9 ya michezo yote 28.
SARE SABA
Katika michezo saba iliyotoka sare, Simba ilianza kwa matokeo ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, kabla ya kutoka 0-0 na Dodoma Jiji, Yanga na Azam FC, huku pia ikitoka 1-1 na Pamba Jiji na TRA United. Sare nyingine ilikuwa 2-2 dhidi ya Yanga, Mei 3, 2026. Matokeo hayo yanaonyesha kwamba hata pale vijana wa Barker waliposhindwa kupata ushindi, waliweza kuepuka kipigo.
WAFUNGAJI
Katika mabao 49 yaliyofungwa na Simba katika mechi 28 za Ligi Kuu Bara chini ya Barker, Clatous Chama ndiye anayeongoza akiwa nayo manane sawa na aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ ambaye sasa yupo Yanga.
Kwa upande mwingine, Elie Mpanzu na Alain Anicet Oura kila mmoja akiwa nayo saba kama ilivyo kwa Libasse Gueye. Beki wa kati, Rushine De Reuck ana mabao matatu, wakati mwenzake Ismael Olivier Toure anayo mawili.
Wafungaji wengine ni Neo Maema, Yusuph Kagoma, Morice Abraham na Inno Jospin Loemba, ambao kila mmoja amefunga bao moja. Bao moja kati ya 49 lilitokana na kujifunga, ambapo Shabani Mgunda alifanya hivyo katika ushindi wa Simba wa 3-0 dhidi ya Fountain Gate.
KWINGINEKO
Wakati hali ikiwa hivyo Ligi Kuu Bara, katika mashindano mengine, Barker ameambulia vipigo viwili. Kocha huyo alianzia Kombe la Mapinduzi 2026 ambapo alishuhudia kikosi kikipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Azam hatua ya nusu fainali. Kabla ya hapo, Barker aliiongoza Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi, kisha 2-1 mbele ya Fufuni ikiwa hatua ya makundi.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ikiwa kundi D msimu uliopita 2025-2026, Barker aliikuta Simba ikiwa tayari imecheza mechi mbili na kupoteza zote dhidi ya Petro de Luanda (1-0) na Stade Malien (2–1).
Baada ya hapo, Barker akaanza na kichapo cha 1-0 dhidi ya Espérance de Tunis, kisha sare ya 2–2 dhidi ya mpinzani huyohuyo.
Sare nyingine ya 1-1 ilifuatia dhidi ya Petro de Luanda, akamaliza na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Stade Malien. Safari ya Simba ikaishia makundi ikiburuza mkia na pointi tano.
Pia, Simba ilishiriki Kombe la Muungano 2026 na kuwa bingwa ikianza kuifunga Mafunzo (1-0), Mlandege (3-0) na Yanga (1-0), huku pia Barker akishinda Kombe la Shirikisho la CRDB ikiifunga Azam bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Gombani.