Simba yaendeleza moto, Coastal bado hakijaeleweka
Muktasari:
- Simba imekusanya pointi 12 kwenye mechi nne ilizocheza baada ya kushinda zote na kukaa kileleni, ikiacha Yanga na pointi tisa iliyocheza mechi tatu katika nafasi ya pili. Wakati huohuo Coastal Union imepoteza mechi ya tatu kati ya nne ilizocheza.
SIMBA imewashusha watani zao wa jadi, Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa Coastal Union bao 1-0, mechi iliyopigwa usiku wa leo Agosti 27, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Simba imekusanya pointi 12 kwenye mechi nne ilizocheza baada ya kushinda zote na kukaa kileleni, ikiacha Yanga na pointi tisa iliyocheza mechi tatu katika nafasi ya pili. Wakati huohuo Coastal Union imepoteza mechi ya tatu kati ya nne ilizocheza.
Bao lililoipa Simba pointi tatu lilifungwa dakika ya 75 na beki wa kati, Ismael Toure akiunganisha kwa kichwa krosi ya Anicet Oura.
Beki wa kulia, Nathaniel Chilambo aliibuka na tuzo ya mchezaji bora baada ya kuonyesha muendelezo wa kiwango kizuri kilichowakosha hadi mashabiki waliohudhuria mechi hiyo.
Mbali na kupewa tuzo hiyo, beki huyo alipongezwa na mashabiki kwa kumpatia fedha.
Hata hivyo, dakika ya 53, baada ya Nathaniel Chilambo kumchezea vibaya Shiza Kichuya, hali haikuwa shwari jukwaani walipokaa wachezaji wa Simba ambao hawakuwa sehemu ya mechi hiyo.
Faulo hiyo iliwafanya Shomari Kapombe, Antony Mligo na Ibraheem Jabaar kuwa na hofu ya pengine mfululizo wa kadi nyekundu ungeelea kuwaandama.
Hofu ilitanda zaidi kwa wachezaji hao baada ya mwamuzi Katanga Hussein kwenda kuangalia kwenye teknolojia ya FVS kujiridhisha uzito wa tukio hilo kama linastahili adhabu ya kadi nyukundu.
Baada ya mwamuzi kujiridhisha, akaamuru ilikuwa ya kawaida, kisha akamuonyesha Chilambo kadi ya njano. Hapo ndipo wachezaji hao wakatulia.
Ikumbukwe hii ni mechi ya nne kwa Simba katika Ligi Kuu Bara msimu huu na tatu zilizotangulia, wachezaji watatu tofauti walionyeshwa kadi nyekundu. Alianza David Kameta 'Duchu' dhidi ya Kagera Sugar, kisha Jabaar (dhidi ya Pamba Jiji) na Mligo (dhidi ya Singida Black Stars).
Kipigo cha leo kwa Coastal Union, kinaendeleza mwendo mbaya wa timu hiyo inayonolewa na Kocha Fikiri Elias ambaye bado hajaonja ladha ya ushindi zaidi ya kukusanya pointi moja kufuatia kupoteza mechi tatu dhidi ya Mashujaa (1-0), Yanga (4-1) na Simba (1-0), huku ikiambulia sare ya 1-1 dhidi ya TRA United.