Mastaa wenye bahati na medali za ubingwa
Muktasari:
- Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya mastaa hao, waliyochukua ubingwa katika timu tofauti za Ligi Kuu hapa nchini na kufanikiwa kupata medali nyingi zinazosalia kama kumbukumbu za maisha yao ya soka.
KUNA baadhi ya wanasoka katika Ligi Kuu Bara, wamekuwa na bahati ya kuvaa medali za ubingwa kila timu wanazokwenda kuzichezea kwa nyakati tofauti.
Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya mastaa hao, waliyochukua ubingwa katika timu tofauti za Ligi Kuu hapa nchini na kufanikiwa kupata medali nyingi zinazosalia kama kumbukumbu za maisha yao ya soka.
Clatous Chama
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama aliyemaliza msimu uliyoisha akiwa na mabao manane, asisti saba ni kati ya mastaa wenye bahati ya kunyakua mataji kwa timu alizocheza hapa nchini.
Baada ya kujiunga na klabu ya Simba mwaka 2018 aliisaidia timu hiyo kuchukua ubingwa msimu 2018/19, 2019/20, 2020/21 kisha akaenda kujiunga na RS Berkane, baadaye akarejea tena Simba.
Pia, Chama kujiunga na Yanga msimu wa 2024/25 pia alichukua ubingwa wa Ligi Kuu, FA akiwa na klabu hiyo, ambapo msimu wa 2025/26 akiwa na Singida BS alichukua taji la Cecafa Kagame cup la mwaka 2025.
Chama amerejea tena Simba kupitia usajili wa dirisha dogo Januari 20, 2026 ambapo kafanikiwa kuvaa medali ya Kombe la Shirikisho la CRDB Cup (FA).
Nickson Kibabage
Beki wa kushoto wa Simba, Nickson Kibabage alianza kuvaa medali za ubingwa akiwa na klabu ya Yanga msimu 2023/24 na 2024/25 ambapo msimu wa 2025/26 aliichezea Singida BS na kuchukua nayo ubingwa wa Cecafa Kagame Cup.
Alipojiunga na klabu ya Simba Januari 20,2026 Kibabage amefanikiwa kuvaa medali ya ubingwa wa Shirikisho la Crdb Cup (FA).
Jonas Mkude
Kiungo mkabaji Jonas Mkude ambaye msimu uliyopita hakuwa na timu, alichukua ubingwa akiwa na klabu ya Simba 2011/12, 2017/18, 2018/19, 2019/20, 2020/21, akiwa na Yanga ilikuwa ni 2023/24 na 2024/25.
Farid Mussa
Winga wa Yanga, Farid Mussa akiwa na klabu hiyo kachukua nayo ubingwa msimu wa 2021/22, 2022/23, 2023/24, 2024/25 na 2025/26 lakini timu ya kwanza kuichezea Azam FC msimu wake wa kwanza kujiunga nayo 2013/14 alichukua nayo ubingwa.
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’
Beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alianza kuchukua mataji ya Ligi Kuu akiwa na Simba msimu wa 2017/18, 2018/19, 2019/20, 2020/21 pia alichukua wa FA 2016/17, 2019/20 na 2020/21 baada ya kujiunga na Yanga msimu 2025/26 pia kavaa medali ya ubingwa.
Khalid Aucho
Kiungo aliyemaliza mkataba wake na Singida BS, Khalid Aucho akiwa na timu hiyo amevaa ya ubingwa wa Cecafa Kagame Cup kwa mwaka 2025, lakini akiwa na Yanga timu ya kwanza kuichezea Ligi Kuu Bara alivaa medali za ubingwa wa ligi msimu wa 2021/22, 2022/23, 2023/24 na 2024/25.
Kutokana na bahati waliyonayo mastaa hao, staa wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma anasema:”Wachezaji hao walikuwa na hesabu nzuri za kujua muda wa kujiunga na timu zinazofanya vizuri na zimewajengea CV nzuri.”
Mwingine aliyetoa mtazamo wake juu ya hilo ni kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule aliyesema:”Walifanya maamuzi sahihi na muda sahii wa kujiunga na timu zilizowapa heshima za kuvaa medali za ubingwa.”