New Amaan Complex wafungwa
Muktasari:
- Katika eneo la Uwanja wa New Amaan Complex, kuna viwanaj vitatu ambapo viwili hutumika kwa ajili ya mazoezi, na mkubwa unaotumika kwa mechi za mashindano mbalimbali.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeufunga kwa muda Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya kurekebisha eneo la kuchezea kwa kupanda nyasi mpya.
Uamuzi wa kufanya hivyo ni kwa ajili ya kuandaliwa kutumika kwa mazoezi kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2027.
Katika eneo la Uwanja wa New Amaan Complex, kuna viwanaj vitatu ambapo viwili hutumika kwa ajili ya mazoezi, na mkubwa unaotumika kwa mechi za mashindano mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir Moh’d Makame, wakati akitoa taarifa kuhusiana na maandalizi kuelekea AFCON 2027.
Amesema, kitakachofanyika ni nyasi za uwanja huo kung’olewa zote na kupandwa mbegu zitakazootesha nyasi mpya ambapo mchakato huo utachukua miezi miwili.
“Uwanja wa New Amaan Complex tumeufunga kwa muda kuimarisha nyasi kwa ajili ya mashindano ya AFCON, tutapanda mbegu mpya na mchakato huo utachukua miezi miwili kupanda, kuota na kuanza kukatwa,” amesema.
Alieleza kuwa, wanafanya hivyo kwasababu Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litafanya ukaguzi na kuanzia Januari 2027, viwanja hivyo vitafanyiwa majaribio.
Naye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai, amesema wamepokea taarifa hiyo ya kufanyiwa ukarabati Uwanja wa New Amaan Complex kwani nyasi hizo zimeshatumika kwa kipindi cha miaka miwili.
Amesema, kwasasa Tanzania ipo katika kuboresha viwanja vyao kwa lengo la kukidhi vigezo na mahitaji ya CAF.
Katibu huyo amesema, taarifa hiyo sio nzuri kiasi kwa upande wao kutokana na muda waliopewa ni ngumu kwa timu za Zanzibar kuutumia kwa mechi zao za kimataifa na Kombe la FA. Amesema, ZFF inafanya mawasiliano na CAF ili kuuangalia Uwanja wa Gombani uliopo Pemba kama utakuwa na vigezo mechi zao zichezwe huko.
Alifafanua kuwa, ikishindikana Gombani, watahitaji mechi hizo zichezwe kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Dar es Salaam.
“Suala la timu zetu kucheza mechi zote mbili nje ya Tanzania mashindano ya Kimataifa na FA sidhani kama lipo katika mpango kwasasa ingawaje tutaangalia faida na hasara.”