Mlandege yaja na sera ya vijana
BAADA ya kutema wachezaji 15, timu ya Mlandege imeanza kushusha mitambo mipya kuelekea msimu wa 2026-2027 huku ikiwa na sera ya kujenga kikosi cha vijana zaidi.
Wachezaji waliotambulishwa katika timu hiyo hadi sasa wengi wao ni vijana chini ya umri miaka 20 ambao ni winga wa kulia Said Seif Said (miaka 17) kutokea Small Simba, beki Amiri Zaid Ali(miaka 20) kutokea Annour Academy, beki Ramadhan Juma (miaka 17) kutoka Dulla Sunday, mshambuliaji Abdul Nassa Michuz (miaka 18) kutokea Inter Zanzibar, kiungo mshambuliaji Muhammed Mustafa (miaka 16) kutoka TMS International Arusha.
Wengine ni kiungo Aver Terlumun Paul (miaka 18) kutoka Flight Football club ya Nigeria, kiungo namba kumi, Mabrouk Ame Fundi (miaka 19) kutoka Wawi, kiungo mkabaji Fahad Hafidh Mohammed (miaka 23) wa Fufuni na beki Abdallah Jumanne Said (miaka 19) wa JKU.
Katibu Mkuu wa Mlandege, Hussein Ahmada, amesema lengo la kusajili vijana msimu huu wanahitaji timu hiyo idumu kwa muda mrefu na kujengwa katika mfumo wa ushindani.
Amesema waanamini vijana ndio wenye uwezo wa kufundishwa na kuelewa kwa haraka na kukaa nao kwa muda mrefu ikilinganishwa na wachezaji wenye umri mkubwa.