Namba sita mpya Yanga hii hapa
Muktasari:
- Yanga ilikuwa kwenye msako wa kiungo mkabaji eneo ambalo bado usajili wake ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo bingwa nchini.
YANGA wakati wowote itaweza kumtambulisha kiungo wake mpya mkabaji, Fred Duval Ngoma, baada ya kufikia makubaliano yote ya msingi.
Yanga ilikuwa kwenye msako wa kiungo mkabaji eneo ambalo bado usajili wake ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo bingwa nchini.
Yanga imefikia makubaliano na klabu ya Olympique de Safi ya Morocco, kwa mauziano ya kiungo huyo mkabaji ikitajwa kutumika kiasi cha Dola 300,000 (Sh792 milioni) kama ada ya uhamisho.
Ngoma ambaye ana kimo cha futi 5.8, atawasili nchini leo mchana tayari kwa kumalizia taratibu za mwisho kujiunga na mabingwa hao wa soka Tanzania.
Kiungo huyo anasifika kwa kazi nzuri ya kupokonya mipira na kuanzisha mashambulizi, ubora ambao umewavutia mabosi wa juu wa Yanga.
Ngoma ambaye ni raia wa Congo-Brazzaville mwenye miaka 28, atajiunga mara moja kwenye kikosi cha Yanga kilichopo kambini, kikiendelea na maandalizi ya msimu ujao wa 2026-2027.
Msimu uliopita Ngoma aliichezea Olympique de Safi jumla ya dakika 2,147 kwenye mechi za mashindano yote akiwa anapata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.
Ngoma anakuja kuchukua nafasi ya Mohammed Damaro ambaye alikuwa akitumikia Yanga miezi sita ya mwisho msimu uliopita, akirudishwa Singida Black Stars alipotoka.