Mwanamke kutoka Uganda ajitosa mashindano ya magari Morogoro
Muktasari:
- Mashindano hayo ya fainali za mbio za magari za African Rally Championship ni ya awamu ya nne na ya mwisho kwa mwaka 2026 ambapo yatahusisha jumla ya magari 23, huku magari manane pekee ndio yatashindania ubingwa wa Afrika, mengine 15 yakishiriki Serengeti Rally of Tanzania.
Susan Muwonge kutoka nchini Uganda, amejitosa kuwa mwanamke wa kwanza Afrika kushiriki fainali za mbio za magari za African Rally Championship 2026 zinazotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 1 hadi 4, 2026, katika maeneo ya Shamba la Miti la TFS, Makundi mkoani Morogoro.
Susan ambaye atashiriki kama dereva rasmi, atakuwa akiendesha gari aina ya Subaru Impreza, huku Musa Nsubuga akiwa dereva msaidizi (co-driver).
Msimamizi mkuu wa mashindano hayo, Dk Mosi Makau, amesema ushiriki wa Susan ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuongeza mvuto wa mashindano hayo na kuendelea kuhamasisha wanawake kushiriki katika mchezo wa mbio za magari.
Msimamizi Mkuu wa Mashindano ya Magari ya Serengeti Rally of Tanzania Dk Mosi Makau, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mashindano hayo yatakayoanza Oktoba 1 hadi 4 katika Shamba la Miti ya la TFS mkoani Morogoro. Picha: Hamida Shariff
"Mashindano haya yatahusisha magari manane huku Tanzania ikiwa na madereva wawili na wengine kutoka Kenya, Zambia, India na Uganda ambapo kwa mara ya kwanza kutakuwa na mwanamke ambaye anashiriki kama dereva, huko nyuma wapo walioshiriki lakini kama madereva wasaidizi lakini huyu ataendesha mwenyewe," amesema Dk Makau.
Amesema mashindano hayo ni ya awamu ya nne na ya mwisho kwa mwaka 2026 ambapo yatahusisha jumla ya magari 23, huku magari manane pekee ndio yatashindania ubingwa wa Afrika, mengine 15 yakishiriki Serengeti Rally of Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mkwawa Group of Company ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Richard Sinamtwa, amesema mashindano hayo ni hatua muhimu katika kukuza mchezo wa magari na kuleta pamoja wadau wa mchezo huo kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mkwawa Group of Company ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano ya magari ya Serengeti Rally of Tanzania, Richard Sinamtwa akieleza faida za mashindano hayo kiuchumi na kiburudani. Picha: Hamida Shariff
Amesema kupitia mashindano hayo ya magari, Tanzania itaendelea kunufaika na ukuzaji wa utalii na uchumi katika jamii ikizingatiwa michezo hiyo inahusiha watu wa mataifa mbalimbali.
"Kupitia mashindano haya tuweze kutunza taswira nzuri ya Tanzania, kupitia michezo tuendeleza kuhamasisha utalii, uhifadhi pamoja na kuhakikisha tunasimamia maendeleo ya jamii zetu," amesema Sinamtwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Tanzania, Satinder Singh Bardi, akieleza namna washiriki wa mashindano ya magari ya Serengeti Rally of Tanzania walivyojiandaa. Picha: Hamida Shariff
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Tanzania, Satinder Singh Bardi, amewataka wakazi wa Morogoro na mashabiki wa mchezo huo kuzingatia usalama wao wakati wote wa mashindano.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kufuata maelekezo ya vyombo vya usalama na kukaa katika maeneo yaliyotengwa kwa watazamaji, ili kuepusha ajali na madhara huku akiwahakikishia mashabiki wa mashindano kuwa yatafanyika kwa usalama.