Mwekezaji Simba aibuka Msumbiji
Muktasari:
- Mo alisema hayo juzi baada kukutana na Rais Daniel Chapo jijini Maputo katika mkutano ambao ulikuwa sehemu ya juhudi za Rais huyo kuhamasisha uwekezaji binafsi kwa ajili ya kukuza uchumi, kuongeza uzalishaji viwandani na kuunda ajira nchini Msumbiji.
RAIS wa Klabu ya Simba Mohammed Dewji (MO) ameahidi kuwekeza dola milioni 250 za Marekani nchini Msumbiji na kusema kampuni yake itajitahidi kuajiri wananchi wa nchi hiyo 20,000.
Mo alisema hayo juzi baada kukutana na Rais Daniel Chapo jijini Maputo katika mkutano ambao ulikuwa sehemu ya juhudi za Rais huyo kuhamasisha uwekezaji binafsi kwa ajili ya kukuza uchumi, kuongeza uzalishaji viwandani na kuunda ajira nchini Msumbiji.
Bilionea huyo Mtanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) alitoa ahadi hiyo baada ya mazungumzo na Rais Chapo akieleza kuwa majadiliano hayo yalikuwa na matokeo mazuri na kwamba ametambua fursa kadhaa za uwekezaji nchini humo.
Ikulu ya Msumbiji ilisema ahadi hiyo inaendana na shughuli mbalimbali za biashara za kundi hilo na inafungua fursa za uwekezaji katika maeneo ya kimkakati, pamoja na kuanzishwa kwa minyororo mipya ya uzalishaji, usambazaji na huduma.
MeTL ni miongoni mwa makampuni makubwa binafsi yenye shughuli mbalimbali nchini Tanzania, ikijihusisha na kilimo, uzalishaji viwandani, usafirishaji na ugavi, nishati, biashara na huduma za kifedha.
Kampuni hiyo mpaka sasa imeajiri takribani watu 37,000 na tayari inafanya biashara katika zaidi ya nchi 12 za Afrika, ikiwemo Msumbiji. Endapo ajira 20,000 zitaongezwa nchini humo, idadi ya wafanyakazi wa kundi hilo itaongezeka kwa zaidi ya nusu.
Dewji, mwenye umri wa miaka 51, alichukua uongozi wa biashara iliyoanzishwa na baba yake, Gulam, katika miaka ya 1970 na kuipanua hadi kwenye uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, zikiwemo nguo, mafuta ya kula, unga, vinywaji na bidhaa za kilimo. Jarida la Forbes linamkadiria kuwa na utajiri wa dola bilioni 2.1, akishika nafasi ya 14 miongoni mwa matajiri barani Afrika na kuwa Mtanzania pekee kwenye orodha hiyo.
Mwanamichezo huyo ambaye amefanikiwa kubadilisha sura ya soka la Tanzania baada ya kuwekeza kwenye klabu ya Simba ambayo kwa kipindi chake zaidi ya miaka saba imeweza kutawala soka la ndani na kuingia kwenye tano bora katika viwango vya Afrika, pia ameiwezesha kutwaa makombe kadhaa ya ndani.
Dewji pia aliwahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kwa vipindi viwili, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, na alikuwa Mtanzania wa kwanza kusaini Giving Pledge, mpango unaowahimiza matajiri duniani kuahidi kutoa sehemu kubwa ya utajiri wao kwa shughuli za kijamii.
Pia anamiliki asilimia 49 ya Simba Sports Club na mwezi huu aliahidi takribani dola milioni 11.3 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na kituo cha mafunzo cha timu hiyo eneo la Bunju ambalo amefanikiwa kuwekeza fedha mara kwa mara kwa ajili ya maboresho na kujenga viwanja vya mazoezini.
Mbali na kuwekeza kwenye miundombinu ya klabu hiyo, MO pia amekuwa akitoa kiwango cha fedha kwa ajili ya kufanya usajili kwenye timu hiyo ambayo hadi sasa imeshacheza michezo mwili ya Ligi Kuu Bara na kushinda yote, ilianza kwa kuichapa Kagera mabao 2-0 na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji.
Hata hivyo, Dewji wala Ikulu ya Msumbiji hawajaweka wazi ratiba ya utekelezaji wa uwekezaji huo wa dola milioni 250, sekta ambazo fedha hizo zitaelekezwa au lini ajira hizo 20,000 zitaanza kuundwa.