Prime
Dewji ni mmiliki, mwekezaji au mfadhili Simba
Wiki moja baada ya sakata la kubatilisha maamuzi ya mkutano mkuu wa Simba lililofichua mgawanyiko mkubwa kati ya upande wa Bodi ya Wakurugenzi na wa uongozi wa klabu, mfanyabiashara anayetangazwa kama mwekezaji, Mohamed Dewji ameibuka na kauli zinazoibua maswali mengi kama ni mwekezaji, mmiliki, mfadhili au mdhamini.
Kauli hizo alizitoa Jumamosi wakati wa tamasha la Simba Day lililofanyika Uwanja wa Uhuru, alipotoa hotuba ndefu inayotetea utoaji wake wa fedha, uwekezaji, kulaumu kuchelewa kumalizika kwa mchakato wa mabadiliko na pendekezo la kukamilisha ujenzi wa uwanja ambao umeshapachikwa jina la Mo Arena ulioko Bunju jijini Dar es salaam.
Wakati fulani Jumamosi, mwenyekiti wa chombo kinachoitwa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crencentius Magori alionekana kama amempokonya kipaza sauti mfadhili huyo katika kile kilichotafsiriwa kuwa kukatiza hotuba hiyo ndefu ambayo baadhi ya maudhui yake yalionekana kutosaili mazingira.
Kama kawaida ya matamasha yaliyopita, Dewji alijitetea kuwa anatoa fedha kufanikisha mipango ya klabu hiyo kongwe katika usajili na mambo mengine, licha ya baadhi ya watu kumlaumu kuwa hatoi.
Pia alielezea ndoto zake za kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Afrika, ndoto za ujenzi wa uwanja bora wa klabu na usajili wa wachezaji bora kutoka kote barani Afrika. Na safari hii alisema ameshaongea na uongozi wa klabiu ya Stuttgart ya Ujerumani ambayo imeahidi kuleta makocha sita watakaoungana na makocha wengine wa Tanzania kuzunguka nchi nzima kusaka wachezaji wenye vipaji ili wote waje Simba.
Kuhusu uwanja, alisema ameshaweka mezani pendekezo la kutoa Sh. bilioni 30 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Mo Arena na kwamba anachosubiri ni Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kuridhia. Hakueleza kama suala hilo lililotokea kwenye bodi au klabu lakini linaonekana linaanza kama lile la Sh. bilioni 20 za kuinunua Simba.
Ulikuwa kama mkutano wa hadhara mbele ya mashabiki walioujaza Uwanja wa Uhuru kusubiri kuona nyota wao waliosajiliwa msimu huu wakionyesha vipaji vyao na jinsi watyakavyoipigania nembo ya Mtaa wa Msimbazi, lakini wakajikuta wakitakiwa kustahimili urefu wa hotuba yenye mengi waliyozoea kuyasikia na ambayo hayakutokea msimu ulipoisha.
Wengi wameanza kuhoji kuhusu hotuba hiyo na nyingine ambazo huwa anazitoa tamasha la Simba Day anapopewa nafasi ya kuzungumza kama mwekezaji katika klabu ambayo haijakamilisha mchakato wa mabadiliko na haijatimiza masharti ya kisheria na kikanuni ya kupata wawekezaji ambao wangechangia kuunda Bodi ya Wakurugenzi yenye uwakilishi wa kila upande; yaani klabu, na kila mwekezaji kutokana na kanuni kutaka idadi ya wawekezaji ianzie wawili.
Kwa hiyo ukiangalia hotuba hiyo iliyojaa mamlaka unaweza kudhani kuwa mchakato ulishakamilika na Dewji ndiye mmiliki halali wa klabu ya Simba kwa kuwa anaweza kuamua muda wa kuweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na bodi ipitishe tu na si kwamba suala hilo liibuliwe na bodi kulingana na umuhimu wake na wakati na kisha ndio kutafutwe wawezeshaji wa ujenzi.
Pia unaweza kuamini kuwa hotuba hiyo imetolewa na mtu ambaye mchakato ulishampitisha kuwa ndiye anamiliki hisa nyingi, kiasi cha kuweza kutangaza mikakati ambayo Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti ya klabu zitalazimika kutekeleza.
Kwamba atoe hotuba iliyojaa mikakati ya klabu kama nani? Mikakati hiyo ilitakiwa itolewe na mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi baada ya kikao kupitisha na itolewe kwa wanahisa (wanachama au uongozi wa klabu, wawekezaji) waliokutana kwenye mkutano wa wanahisa au mkutano mkuu badala ya mashabiki waliofuata burudani Uwanja wa Uhuru.
Na hotuba hiyo maana yake uongozi wa klabu unatakiwa kwenda kuitekeleza na kwa maana nyingine irudi kwa mashabiki kuwaambia ilipofikia kwenye utekelezaji badala ya kurudi kwa wanahisa au wanachama. Kwa lugha rahisi amejikinga na ngao huku kuwarishia mpira viongozi wa bodi.
Ndio maana mwenyekiti wa klabu, Murtazar Mangungu hakupewa nafasi ya kugusa kipaza sauti kama mtu anayetoka upande wa wenye hisa chache, kumbe kwa nafasi yake ndiye nguzo ya Simba.
Pia utaweza kudhani kuwa Mo Dewji ndiye mfadhili mkuu wa klabu ya Simba ambaye kila msimu husaidia kutoa fedha kwa ajili ya usajili au kushughulikia masuala yanayojitokeza klabuni. Kwamba anajitetea kiwa huwa anatoa fedha kama nani? Kama mwekezaji au mfadhili au mdhamini?
Huku jezi ya Simba ikiwa na matangazo kadhaa ya bidhaa za kampuni yake ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL), Dewji hujiepusha kabisa kuzungumzia suala hilo la nembo za bidhaa zake kuonekana kwenye jezi za Simba.
Nembo za bidhaa hizo, ambazo baadhi ziko kifuani, zinamaanisha fedha nyingi kuingia Simba kutoka kwa watengenezaji. Hapo humsikii dewji akizungumzia bidhaa hizo.
Unapojiuliza hayo ndipo unapata swali jingine kwamba kwani Simba ilifanya mabadiliko ya muundo na umiliki ili iweje? Kwa ajili ya kutaka Mo Dewji awe anatoa fedha kila wakati zinapohitajika? Awe anatoa mwelekeo wa klabu badala ya viongozi? Awe anaanzisha mipango ya maendeleo ndipo viongozi waitekeleze kwa kumuangalia?
Au ilifanya mabadiliko ili ijiimarishe kiuchumi na kuwezesha watu wengi wenye fedha kuvutiwa na muundo na kutaka kuwekeza ili wanufaike na umaarufu wa klabu na uwezo wao uwanjani?
Tangu Brazil ikamilishe sheria ya 14,193/2021 maarufu kwa jina la SAF (Sociedade Anonimo do Futebol), ambayo ilijenga mazingira ya klabu za soka zilizokuwa zinamilikiwa na wanachama kugeuka na kuwa za kutengeneza faida, klabu za nchi hiyo zimevutia wawekezaji na kuimarika kiuchumi.
Baadhi ya mashirika au kampuni kubwa za barani Ulaya zimenunua klabu za Brazil na kuziunganisha kwenye mitandao yao mikubwa duniani ya klabu za michezo na hivyo sasa si rahisi kuchukua mchezaji nyota Brazil kwa bei rahisi.
Pamoja na kwamba mageuzi hayo yalichangiwa na sheria za nchi, mantiki kubwa hapo ni kufanya mabadiliko yanayolenga kuzifanya klabu zijiendeshe kibiashara na kuondokana na utegemezi.
Mwekezaji aingie kwenye klabu kwa kuweka fedha zake na kusubiri matunda na si kuingia kwenye mikutano na wanachama kujaribu kujijengea taswira nzuri na kuwashtaki viongozi kwa wanachama na zaidi ya yote kutaka kuonyesha kuwa bila ya yeye klabu haiwezi kusonga mbele.
Ni muhimu Mo Dewji akabainisha anataka kuwa upande gani kwenye mageuzi ya Simba. Kama amefurahishwa na mageuzi na hivyo anataka kusaidia kwa kuwa mfadhili anayeweza kutoa fedha wakati wowote kutokana na mapenzi yake, basi ijulikane wazi ili hata pale asipotoa asilaumiwe.
Kama anataka kweli kuwa mwekezaji kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na nchi, basi asubiri mchakato ukamilike ili aweke fedha zake halafu ziingizwe kwenye mtaji wa klabu na baadaye asubiri gawio. Lakini hadi sasa Sh. bilioni 20 alizosema kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa amelipa ili kununua asilimia 49 za hisa, bado hazijawekwa klabuni na kwa mujibu wa Magori, ziko kwenye akaunti ya escrow na hivyo mamlaka aliyoyaonyesha juzi kwa sasa hanayo.
Na kama anataka kuwa mdhamini, basi ajikite katika kuimarisha udhamini wake na ikiwezekana awe mdhamini mkuu anayeweka bidhaa yake kifuani badala ya mdhamini wa sasa wa Simba ambaye ni Betway.
Lakini kama anataka kuwa mmiliki kamili, hilo haliwezekani kwa sasa nchini kwa klabu zinazomilikiwa na wanachama. Kuondokana na ulazima wa kujitetea kila mwaka, kukashifiwa, kulaumiwa na mengine, Dewji hana budi kuanzisha timu nyingine kama ilivokuwa wakati alipoinunua Singida United.