Mwamuzi wa Gwambina v Simba apigwa ‘stop’
Muktasari:
Mwamuzi Godfrey Msakila aliyechezesha mchezo wa Gwambina dhidi ya Simba ameondolewa katika ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo huo.
Mwamuzi Godfrey Msakila aliyechezesha mchezo wa Gwambina dhidi ya Simba ameondolewa katika ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo kati ya Simba na Gwambina.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 28, 2021 na Idara ya Habari na Mawasiliano Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imesema kuwa adhabu hiyo imetolewa baada ya kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) cha Aprili 27, 2021 cha kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Mchezo huo Namba 185 kati ya wenyeji Gwambina FC dhidi ya Simba SC uliochezwa Aprili 24, 2021 kwenye uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza ambapo Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, “Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 40:1(2.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi”.