Ahmed Ally: Tunamtakia kila la heri Mwalimu, Simba ipo imara
Muktasari:
- Simba itakutana na Yanga kesho katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Wakati Simba ikimaliza mazoezi yake ya mwisho usiku huu kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Meneja wa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema maandalizi yamekwenda vizuri na hakuna jambo lililowatingisha.
Simba itakutana na Yanga kesho katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Ahmed amesema hali ya kambi ya timu hiyo ni salama na hakuna jambo lililowaondolea utulivu kiufundi, licha ya kuondoka kwa aliyekuwa mshambuliaji wao, Seleman Mwalimu.
“Kila kitu kuhusu maandalizi yetu kimekwenda vizuri. Tangu tumefika hapa Zanzibar tumepata vipindi viwili vya mazoezi na ninachowathibitishia Wanasimba ni kwamba tupo sawasawa kwenda kuipigania Simba,” amesema Ahmed.
“Kambi yetu ipo salama, hatuna sababu ya kupata wasiwasi. Kila kitu kuhusu ufundi kinakwenda sawasawa, hakuna ambacho kimetuathiri kwa namna yoyote. Kama kuna makelele, hatujayaruhusu kuingia kwenye timu yetu.”
Kauli hiyo imekuja baada ya Mwalimu kuondoka kambini usiku mara baada ya mazoezi ya juzi usiku akaenda kukamilisha usajili wa kujiunga na Yanga.
Ahmed amesema Simba inamtakia kila la heri mchezaji huto katika safari yake mpya ya soka, baada ya kujiunga na klabu aliyoichagua, huku akisisitiza kuwa kwa sasa uongozi wa klabu hiyo unajipanga kukamilisha usajili wake na siyo kufanya “malipizi”.
“Simba tunamtakia kila la heri Mwalimu wakati anapojiunga na klabu aliyoichagua. Simba tupo imara. Kwa sasa uongozi unaendelea kujipanga kumaliza usajili kabla ya dirisha kufungwa, kulingana na mahitaji yetu," amesema.
“Hatuwezi kufanya malipizi. Hizo zitakuwa ni hesabu za muda mfupi, lakini tutatuliza akili kuhakikisha tunakamilisha mahitaji yetu ya kiufundi sokoni kwa mujibu wa malengo yetu."