Prime
Mtego wa Sh260 milioni waisubiri Simba
SIMBA imeshatua Malawi ikiwa gumzo kubwa nchini humo ikitarajiwa kuanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Mighty Wanderers sasa kocha wa wekundu hao Steve Barker amenyoosha maelezo akisema safari hii hawataki mazoea, huku wenyeji wao wakiwekewa kitita mezani.
Msimu uliopita, Simba kiujumla kuanzia hatua ya mtoano ya awali mpaka makundi ya Ligi ya Mabingwa ilicheza jumla ya mechi 10 katika hizo ilishinda tatu, ikapoteza tatu, ikitoa sare nne, ikifunga mabao 10 na kuruhusu manane.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema msimu huu wanataka kuanza kwa nguvu kubwa kampeni yao hiyo, akiringia ubora wa kikosi chake akidai kwamba kina uwezo wa kushinda mechi hizo kubwa Afrika.
Barker amesema msimu uliopita ulikuwa na sura mbili ambapo aliikuta timu hiyo ikiwa imeshaanza mechi za hatua ya makundi ambapo alipambana kuhakikisha wanasitisha matokeo ya kupoteza lakini baadaye pointi hazikutosha.
“Tupo tayari kuanza msimu huu wa ligi ya Mabingwa Afrika, haitakuwa rahisi sana lakini tumejipanga kufuta kile ambacho kilitupa shida msimu uliopita, kama unakumbuka niliikuta timu ikiwa imeshaanza mashindano,”amesema Barker.
“Ikiwa imepoteza mechi mbili, tukapoteza tena ya tatu lakini niliwaambia wachezaji kwamba tunatakiwa kuzuia matokeo ya namna hiyo, tukafanikiwa lakini hatukuweza kukusanya pointi za kutosha, msimu huu tunataka kucheza kwa viwango vya Simba.
“Kila mchezo utakuwa na umakini mkubwa, hakuna timu ambayo itadharaulika, huku wanacheza wale ambao walifanya vizuri kwenye mataifa yao, tuna kikosi imara ambacho kinaweza kutupa matokeo mazuri amesema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
Aidha Barker amesema sura ya pili ya kikosi chake ilikuwa kukiongezea nguvu ambapo kazi hiyo ilifanyika katika madirisha mawili yaliyopita ya usajili ambapo anaamini kwamba maboresho hayo yataipa matokeo chanya.
“Nilipofika tulifanya uisajili mkubwa katika dirisha la usajili la Januari, lilitupa wachezaji bora ambao walituiongezea thamani kubwa, hili dirisha lililopita tulichofanya ni kuongezea nguvu wapo wachezaji ambao wameshaanza kufanya vizuri na wengine ni suala la muda tu watathibitisha kwamba wana thamani ya kuwa hapa.
“Tuna nguvu kubwa ya mashabiki wetu, tuna jukumu la kuwapa furaha ambayo wanaitarajia kwetu, tutacheza kama ambavyo Simba anatakiwa kucheza kwa nguvu yake, hatutakuwa na chaguo, kwetu kushinda haitatakiwa kuangalia tunacheza nyumbani au ugenini.”
Hata hivyo, baada ya Simba kufika Malawi wamekutana na stori ya wadhamini wa timu hiyo kuweka kitita cha dola 100,000 zaidi ya shilingi milioni 260 endapo timu hiyo ya Malawi itafanikiwa kuibuka na ushindi jambo ambalo ni mtengo kwa vijana hao wa Msimbazi.