KAZI IPO! Miamba ya Afrika yasaka heshima, Simba na Yanga zatajwa
Muktasari:
- Ni klabu zilizofanya makubwa katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika na msimu huu kazi ipo kwenye kusaka ubingwa.
MSIMU wa 2026/27 wa michuano ya klabu Afrika imeanza jana kwa baadhi ya mechi kupigwa huku macho na masikio yakiwa kwa timu vigogo zinazopambana kurejesha heshima zao.
Al Ahly ya Misri, Raja Casablanca ya Morocco, TP Mazembe ya DR Congo, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia ni kati ya timu zinazoangaliwa zaidi na zinaingia zikiwa na presha ya kurejesha heshima zao.
Ni klabu zilizofanya makubwa katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika na msimu huu kazi ipo kwenye kusaka ubingwa.
TP Mazembe, ASEC Mimosas na Club Africain zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Al Ahly na Raja Casablanca ziliangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushindwa kutamba katika ligi zao za ndani.
AL AHLY
Ndiyo timu yenye mafanikio zaidi Afrika katika michuano ya CAF na msimu huu itacheza Shirikisho.
Imebeba taji la Ligi ya Mbaingwa Afrika mara 12 na iliwashtua wengi kusikia msimu huu itacheza Shirikisho kwani si kawaida kwa miamba hii ya Cairo, Misri.
Itaanzia hatua ya pili ya mchujo dhidia ya mshindi wa mechi kati ya Mogadishu City Club ya Somalia na Kitara FC ya Uganda.
Baada ya kukosa kushiriki Ligi ya Mabingwa, Al Ahly inataka kudhihirisha ubabe wake Afrika na itakwenda kuitingisha Shirikisho katika kuzisaka Dola 4 milioni za mshindi wa kwanza.
RAJA CASABLANCA
Kama ilivyo Al Ahly, miamba hii ya jiji la Casablanca imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuzingua katika kusaka ubingwa wa Morocco uliokwenda MAS Fez.
Raja imetwaa ubingwa wa Afrika mara tatu na ni moja ya klabu zinazoheshimika zaidi kutokana na mafanikio hayo.
Katika michuano ya Shirikisho itaanzia hatua ya pili ya mchujo na itakutana na mshindi kati ya El Kanemi Warriors ya Nigeria na UDIB ya Guinea-Bissau.
Katika michuano hii imebeba mara mbili katika ushiriki wao wa mara tano, hivyo ina uzoefu nayo na ni moja ya timu zinazopewa nafasi ikitumia michuano hiyo kurejesha kujiamini.
TP MAZEMBE
Miamba ya Lubumbashi imetwaa ubingwa wa Afrika mara tano na imewahi kutawala soka la kwa kipindi kirefu na kuacha alama kubwa kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa.
Safari yao msimu huu inaanza kwenye hatua ya kwanza ya mchujo dhidi ya Medeama SC ya Ghana na endap[o itavuka, itakutana na mshindi kati ya Club Africain ya Tunisia na Djoliba AC ya Mali katika hatua ya pili ya mchujo, wakisaka tiketi ya kwenda hatua ya makundi.
Lubumbashi bado ni moja ya sehemu ngumu kwa wapinzani kusafiri kwenda kucheza, huku uzoefu wa Mazembe kwenye mashindano ya bara ukiwa silaha muhimu.
ASEC MIMOSAS
Miamba hii ya Ivory Coast ilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1998 na kwa muda mrefu imekuwa ikiheshimika kutokana na mfumo wake wa kulea vipaji ambavyo vimefika mbali kuanzia ngazi ya klabu na timu za taifa.
Itaianza safari yake katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ugenini dhidi ya ASCK ya Togo na endapo itavuka, itakutana na mshindi kati ya MAS de Fès ya Morocco na Rahimo FC ya Burkina Faso katika hatua ya pili ya mchujo.
Inasaka kufika hatua ya makundi ili kurejea kuwa moja ya klabu vigogo Afrika ikichagizwa na mfumo wake wa kukuza vipaji huku vingi vikiisaidia kufikia mafanikio kabla ya kusaka malisho kwengine.
CLUB AFRICAIN
Ni vigumu kutaja historia ya soka la Tunisia bila kuligusa jina la Club Africain.
Miamba hiyo ya Tunis ilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1991 na kuwa klabu ya kwanza kutoka chini hiyo kushinda mashindano makubwa zaidi ya klabu Afrika.
Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni imekuwa ya misukosuko na kutokuwa na mwendelezo, wakati wapinzani wao wakubwa, Espérance, wamekuwa wakitawala zaidi Tunisia na kwenye mashindano ya Afrika.
Sasa kurejea Ligi ya Mabingwa kunawaletea nafasi kubwa pamoja na presha.
Club Africain itaanza dhidi ya Djoliba AC ya Mali katika hatua ya kwanza ya mchujo na ikipita itakutana na ugumu mbele ya TP Mazembe, iwapo vigogo hao wa DR Congo wataitoa Medeama.
Iwapo hilo litatokea, Club Africain na Mazembe watakutana katika pambano la mabingwa wawili wa zamani wa Afrika kabla hata hatua ya makundi haijaanza.
Hilo linaonyesha jinsi safari ya kufuzu ilivyo ngumu msimu huu.
Kwa Club Africain, kufika mbali hakutakuwa tu suala la mafanikio ya michezo. Kunaweza kuwa mwanzo wa kurejesha kujiamini ndani ya klabu na kuanza tena safari ya kurudi kwenye kundi la vigogo wa Tunisia na Afrika.
SIMBA SC – TANZANIA
Simba SC ni miongoni mwa klabu za Tanzania ambazo zimekuwa karibu zaidi na kubeba taji la Afrika, lakini imekosa bahati hiyo mara mbili.
Timu hiyo ambayo ina rekodi kubwa kwenye michuano ya Caf imewahi kufika fainali ya mashindano ya CAF mara mbili, lakini kila safari imeishia kwenye maumivu.
Mwaka 1993, Simba ilifika fainali ya CAF Cup, lakini ikachapwa na Stella Club d’Adjamé ya Ivory Coast.
Baada ya kusubiri zaidi ya miongo mitatu, Simba ilirudi tena kwenye fainali ya CAF mwaka 2025, safari hii katika Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, RS Berkane ya Morocco iliivuruga ndoto hiyo kwa kuibuka mshindi wa jumla ya mabao 3-1.
Simba pia ina historia ya kufika nusu fainali ya African Cup of Champions Clubs mwaka 1974, inakwenda tena kwenye michuano ya mwaka huu ikiwa na kikosi kipya, kocha mpya imani mpya kutoka kwa mashabiki wao.
YANGA – TANZANIA
Yanga ilipata nafasi nzuri zaidi ya kutwaa taji la Afrika mwaka 2023 ilivyofika fainali ya Kombe la Shirikisho.
Yanga ilipoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria. Lakini ilifanya kazi kubwa ugenini kwa kushinda 1-0 Algeria.
Matokeo ya jumla yalikuwa 2-2, lakini USM Alger ikanyakua ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini.
Hadi sasa, hiyo ndiyo fainali pekee ya mashindano ya juu ya CAF ambayo Yanga imewahi kucheza na msimu huu imekuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi na kocha, tusubiri tuone.