Kadi nyekundu ya Gibrilla Sillah yafutwa
Muktasari:
- Leo Bodi katika kurasa zake ilitoa taarifa; “Kamati ya uendeshaji na usimamii wa ligi imefuta adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji Gibrill Silla katika mchezo namba 034 baada ya kujiridhisha kupitia picha jongeo na taarifa ya wataalamu kuwa mchezaji huyo hakustahili adhabu hiyo.”
BAADA ya Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge kuibua hoja kuhusu kadi nyekundu aliyopewa mchezaji wake, Gibrilla Sillah, akilinganisha na namna tukio lenyewe lilivyotokea uwanjani, Bodi ya Ligi Kuu Bara imetoa taarifa ya kufutwa kwa adhabu hiyo.
Kiungo mshambuliaji huyo alipewa kadi nyekundu kwa kosa ambalo mwamuzi alitafsiri ni kumchezea madhambi mchezaji wa Kagera Sugar beki Evastus Jali.
Leo Bodi katika kurasa zake ilitoa taarifa; “Kamati ya uendeshaji na usimamii wa ligi imefuta adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji Gibrill Silla katika mchezo namba 034 baada ya kujiridhisha kupitia picha jongeo na taarifa ya wataalamu kuwa mchezaji huyo hakustahili adhabu hiyo.”
Sasa Ibenge atakuwa huru kumtumia kiungo huyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na ligi ya ndani na Azam itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya mshindi wa mechi kati ya ZED FC ya Misri na ASAS Djibouti Télécom ya Djibouti.
Mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo, Greyson Buchard kutoka Kagera, amepewa onyo kali kwa kuonyesha mapungufu katika kutafsiri sheria za soka.
Azam pia imepewa onyo kali baada ya kushindwa kuwakilishwa na kocha msaidizi kwenye mkutano na wanahabari siku moja kabla ya mechi, jambo lililokiuka Kanuni ya 17:57 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Michezo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza ametozwa faini ya Sh10 miliono kwa kosa la kushutumu na kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi katika mechi dhidi ya Simba.
Meneja wa Nashindano wa Singida, Tabitha Kidawawa shauri lake lemepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kutokana na makosa ya kujirudiarudia ya kimaadili katika mechi za nyumbani za ligi hiyo.
Pia afisa kutoka idara hiyo, Pablo Almasi ametozwa faini kama hiyo kwa kosa la kusambaza machapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram ya kumkashifu mwamuzi wa mechi hiyo, huku pia akiikebehi teknolojia ya Football Video Support (FVS), katika mechi ya Yanga dhidi ya Coastal Union.
Adhabu nyingine iliiangukia Polisi Tanzania iliyotozwa faini ya Sh10 milioni kwa kosa la kumjumuisha mchezaji mmoja pekee kutoka timu ya vijana kwenye orodha ya wachezaji 21 ikiwa ni na kanuni za ligi.
Kamati hiyo pia imemfutia adhabu ya kufungiwa miezi 12 aliyekuwa Kocha Mkuu wa IAA, John Zongwe ambaye tayari alikuwa ametumikia miezi sita. Kocha huyo aliwasilisha ombi la kupunguziwa adhabu hiyo na kuahidi kuwa balozi mzuri kwa makocha wengine.
Pia kamati hiyo imeipa onyo kali Geita Gold kwa kosa la maafisa wake kuchelewa dakika 15 kufika katika kikao cha kitaalamu cha maandalizi na utaratibu wa mechi dhidi ya Simba, huku Namungo ikipewa onyo kali kwa kuchelewa kufika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam kucheza dhidi ya JKT Tanzania Agosti 29.