Prime
Kocha Gaborone United aingiwa hofu
BAADA ya misimu minne mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikivuka hatua ya kwanza, Yanga SC leo inaingia uwanjani ikiwa na mtihani mwingine wa kuendeleza mwenendo huo, safari hii ikikabiliana na Gaborone United ya Botswana katika hatua ya kwanza ya mashindano hayo msimu wa 2026-2027.
Hii ni hatua ambayo inakwenda kuupima ubora wa Yanga ile inayoonekana kwenye Ligi Kuu Bara kama utafanana na ule wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni mchezo kati ya timu yenye uzoefu mkubwa kwenye michuano hii, yaani Yanga dhidi ya timu inayojitafuta, kama watacheza kama walivyocheza dhidi ya Simba msimu uliopita mashabiki watarajie mchezo bora sana.
Siyo mechi ya historia, wala siyo mechi ya kutafuta majina bali kupata ushindi na kufuzu kwenda hatua inayofuata ndiyo heshima ambayo mashabiki wa Yanga wanaisubiri leo usiku.
Yanga inaanza safari hiyo ikicheza dhidi ya Gaborone United kuanzia saa 2:00 usiku kwa saa za Tanzania kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Botswana, kabla ya timu hizo kurudiana Septemba 12, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo unakuja wakati Yanga ikiwa na kumbukumbu inayoipa matumaini makubwa, hasa ikizingatiwa tangu ilipoondolewa katika hatua ya kwanza msimu wa 2021-2022, haijawahi tena kushindwa katika hatua hiyo ya mwanzo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, rekodi hiyo nzuri ndiyo inayoweza kuufanya mchezo dhidi ya Gaborone kuwa na uzito zaidi kwa Yanga.
Mabingwa hao wa Tanzania hawataangalia tu kuvuka hatua ya kwanza, bali wanataka kuanza safari ya kurejea kwenye hatua ya makundi na zaidi ya hapo kutimiza malengo ya kucheza hatua ya nusu fainali msimu huu.
YANGA ILIPOANZA NA ILIPOFIKA
Msimu wa 2021-2022, ndio ulikuwa wa mwisho kwa Yanga kushindwa kuvuka hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ilikutana na Rivers United ya Nigeria, ikapoteza mechi zote mbili kwa matokeo ya 1-0 nyumbani na 1-0 ugenini.
Huo ulikuwa mwanzo wa kipindi ambacho Yanga ilianza kujijenga upya katika mashindano ya kimataifa, na misimu iliyofuata ikaonyesha tofauti katika uwezo wake wa kuvuka hatua za mwanzo.
Msimu wa 2022-2023, ilianza kwa kuifunga Zalan ya Sudan Kusini mabao 4-0, Septemba 10, 2022, kabla ya kuichapa 5-0 mechi ya marudiano Septemba 17. Licha ya kuvuka hatua hiyo, safari yake iliishia mtoano wa kuwania kufuzu makundi. Baada ya hapo ilidondokea Kombe la Shirikisho Afrika na kwenda hadi fainali.
Msimu uliofuata, 2023-2024, Yanga iliendelea kuonyesha ubora wake. Ilianza kwa kuifunga Djibouti Telecom mabao 2-0, Agosti 20, 2023, kabla ya kushinda 5-1, Agosti 26.
Safari hiyo ilienda mbali zaidi hadi hatua ya robo fainali na Yanga ilikutana na Mamelodi Sundowns. Mechi zote mbili ziliisha kwa suluhu ya 0-0, lakini Yanga ikaondolewa kwa penalti 3-2 na kukosa nafasi ya kutinga nusu fainali.
Msimu wa 2024-2025, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi katika hatua ya kwanza na kuonyesha tena tofauti ya viwango. Ilishinda 4-0 ugenini, Agosti 17, 2024, kisha ikamaliza kazi kwa ushindi wa 6-0 nyumbani, Agosti 24. Msimu huo ilifika hatua ya makundi na kumaliza nafasi ya tatu Kundi A. Safari ikaishia hapo.
Msimu wa 2025-2026, Yanga iliendeleza mwenendo huo dhidi ya Wiliete ya Angola. Iliibuka na ushindi wa 3-0 ugenini Septemba 19, 2025 na kushinda 2-0 katika mchezo wa marudiano Septemba 27. Iliingia hatua ya makundi na kumaliza nafasi ya tatu Kundi B. Safari ikaishia hapo.
Rekodi hiyo inaonyesha jambo moja muhimu, Yanga imebadilika katika miaka ya hivi karibuni. Kutoka kuondolewa hatua ya kwanza msimu wa 2021-2022, imekuwa ikivuka hatua hiyo katika misimu iliyofuata na kuingia kwenye ushindani mkubwa zaidi. Sasa swali linabaki, Gaborone inaweza kuvunja mwenendo huo au itaendelea kuiacha Yanga kufanya inavyofanya siku zote? Tusubiri tuone.
GABORONE INA KAZI
Kwa upande mwingine, Gaborone inaingia katika mechi hii ikiwa haina mwendelezo mzuri katika mashindano ya CAF kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Katika misimu hiyo, imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili na Kombe la Shirikisho Afrika mara moja, lakini haijawahi kufika hatua ya makundi.
Msimu wa 2022-2023, Gaborone ilianza Ligi ya Mabingwa kwa kuifunga AS Vita Club ya DR Congo 1-0 nyumbani Septemba 11, 2022, lakini ikapoteza 3-1 ugenini wiki moja baadaye na kuondolewa.
Msimu wa 2023-2024, ilihamia Kombe la Shirikisho Afrika. Iliifunga Elgeco Plus ya Madagascar 1-0 nyumbani na 3-1 ugenini, kabla ya kukutana na SuperSport United ya Afrika Kusini katika hatua iliyofuata.
Gaborone ilitoka sare ya 1-1 nyumbani Septemba 16, 2023, lakini ikapoteza 3-0 ugenini Septemba 29 na kuishia hatua ya pili.
Msimu wa 2025-2026, ilirejea Ligi ya Mabingwa Afrika na kukutana na Simba SC ya Tanzania. Gaborone ilipoteza 1-0 nyumbani Septemba 20, 2025, kabla ya kupata sare ya 1-1 katika mechi ya marudiano Septemba 28 na kuondolewa.
Kwa maana hiyo, katika misimu mitano iliyopita, Gaborone haijafika makundi. Hilo linaipa Yanga uzoefu mkubwa zaidi wa mashindano ya ngazi hii, pia linaweza kuwa eneo ambalo Gaborone itajaribu kulitumia kujenga historia mpya.
KAULI YA MANQOBA MNGQITHI
Yanga haionekani kuwa na mpango wa kwenda Botswana kucheza kwa tahadhari kupita kiasi. Kocha wake, Manqoba Mngqithi amesema amefanya utafiti wa kina kuhusu wapinzani hao na anajua umuhimu wa kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza.
“Hatuidharau Gaborone hata kidogo, tunakwenda kuikabili na tahadhari kubwa. Kitu ninachoweza kuhakikisha ni hatutacheza kwa lengo la kuzuia, tutakwenda kushambulia,” amesema Mngqithi.
Kwa upande wa Gaborone, kocha wake, Sean Connor, amesema anafahamu ukubwa wa kazi iliyo mbele yake baada ya kufanya utafiti kuhusu Yanga kupitia watu wake anaowafahamu Tanzania.
“Tunakwenda kukutana na timu nzuri yenye jina kubwa Afrika. Baada ya kupangwa kwa ratiba hii, nilianza kazi ya kuwafuatilia. Kuna rafiki zangu wamenipa taarifa za kutosha kuhusu wao (Yanga), tunatakiwa kujipanga sawasawa,” amesema Connor.
“Ukiiangalia kwenye makaratasi utaona wana safu nzuri ya ushambuliaji, wamekuwa kwenye joto zuri kwenye ligi ya nyumbani. Huwezi kuona ni timu rahisi unayokutana nayo ikiwa na mshambuliaji kama Peter Shalulile,” amesema na kuongeza.
“Ukiangalia eneo la kiungo nako wana wachezaji wazuri. Nimeona kuna kiungo kutoka Kongo, Maxi (Nzengeli), ni mchezaji mwenye nishati ya kutosha akiwa uwanjani, lakini wana Aziz KI, ni mmoja kati ya viungo bora Afrika. Unapotakiwa kushindana na timu ya namna hiyo lazima uwe na mpango wa kuwafanya wasicheze kwa uhuru wao.”