Mtasingwa Adolf usajili wa bilioni
Muktasari:
- Mtasingwa mwenye umri wa miaka 27, alijiunga rasmi na Kaizer Chiefs juzi, huku akiandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza raia wa Tanzania kuitumikia timu hiyo kongwe nchini humo.
UHAMISHO wa kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa Dola 500,000 (Sh1.3 bilioni) kutoka Azam FC unamfanya kiungo Adolf Mtasingwa sasa kuwa mchezaji wa tatu wa Kitanzania aliyehamishwa kwa kiasi kikubwa cha fedha kulinganisha na wengine.
Mtasingwa mwenye umri wa miaka 27, alijiunga rasmi na Kaizer Chiefs juzi, huku akiandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza raia wa Tanzania kuitumikia timu hiyo kongwe nchini humo.
Chanzo cha uhakika ndani ya Azam FC kimelithibitishia gazeti hili kwamba mchezaji huyo ameuzwa kwa dau la Dola 500,000 ambalo lilifanya wasisite kumuachia.
“Suala la kumuuza Adolf halikuangalia tu fedha ambayo Azam FC tunapata, bali pia maslahi binafsi ya mchezaji. Atalipwa kiasi kikubwa cha mshahara kule ambacho kitamfanya awe miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania mamilionea.
“Sisi tunamtakia kila la kheri na tunaamini usajili wake utafungua milango kwa wachezaji wengine wa Tanzania hasa wa Azam FC nchini Afrika Kusini,” kilifichua chanzo hicho.
Kwa uhamisho huo, Mtasingwa anaingia katika orodha ya wachezaji watatu wa Kitanzania waliowahi kununuliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.
Anayeongoza ni Mbwana Samatta ambaye mwaka 2020 alinunuliwa kwa kiasi cha Euro 20 milioni (Sh60 bilioni), kutoka Genk kwenda Aston Villa.
Mchezaji anayeshika nafasi ya pili ni Novatus Miroshi ambaye uhamisho wake kutoka Zulte Weregem kwenda Goztepe mwaka 2024, uligharimu kiasi cha Euro 700,000 (Sh2.1 bilioni).
Mtasingwa yuko nafasi ya tatu kwa kununuliwa kwa Sh1.3 bilioni na anayeshika nafasi ya nne ni Saimon Msuva kutokana na uhamisho wake wa Euro 287,000 (Sh849 milioni) kutoka Difaa El Jadida kwenda Wydad Casablanca mwaka 2020.
Mchezaji anayeshika nafasi ya tano kwa uhamisho wa gharama kubwa ni Kibu Denis ambaye mwanzoni mwa mwaka huu, Simba ilimuuza kwenda Al Nasr ya Libya kwa dau la Dola 300,000 (Sh792 milioni).
Akizumgumzia uhamisho wake kwenda Kaizer Chiefs, Mtasingwa amesema kwamba ni jambo la kipekee.
“Namshukuru Mungu kwa jambo hili. Naishukuru klabu yangu ya Azam FC kwa kuruhusu nijiunge na Kaizer Chiefs, naishukuru familia yangu na wote ambao wamekuwa wakiniunga mkono.
“Kujiunga na Kaizer Chiefs ni jambo la heshima hivyo nitajitahidi kuhakikisha timu yangu mpya inafanya vizuri,” amesema Mtasingwa.