Azam yaitandika Dodoma Jiji Fei Toto akikosa ufungaji bora
Muktasari:
- Wakati Azam ikiondoka na ushindi huo, kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' aliyekuwa kinara wa ufungaji mabao kwa muda mrefu, amejikuta akizidiwa na Mosi Nduwumwe wa Singida Black Stars aliyemaliza na mabao 17 baada ya leo kufunga mabao matatu 'hat trick' wakati Singida ikichapwa 4-3 na Fountain Gate.
MABAO mawili yaliyofungwa na Jean-Jacques Ngita dakika ya 66 na Nathaniel Chilambo dakika ya 89 dhidi ya Dodoma Jiji, yameifanya Azam kumaliza msimu kwa ushindi huo ikikomaa nafasi ya tatu ikikusanya pointi 62.
Wakati Azam ikiondoka na ushindi huo, kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' aliyekuwa kinara wa ufungaji mabao kwa muda mrefu, amejikuta akizidiwa na Mosi Nduwumwe wa Singida Black Stars aliyemaliza na mabao 17 baada ya leo kufunga mabao matatu 'hat trick' wakati Singida ikichapwa 4-3 na Fountain Gate.
Katika mechi ya leo kuhitimisha msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC 2026-2027, Azam ilikuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, huku Fei Toto mwenye mabao 15, akianzia benchi.
Kipindi cha kwanza, Dodoma Jiji ilifanya mabadiliko ya lazima kipindi cha kwanza baada ya kumuingiza Beno Ngassa dakika ya 39 akichukua nafasi ya Idd Kipwagile aliyeumia.
Kwa Azam, ilifanya mabadiliko dakika ya 63 ilipomtoa beki Laundry Zouzou na kumuingiza Lusajo Mwaikenda, Abdul Suleiman akampisha Idd Seleman, huku Adolf Mtasingwa akimpisha Fei Toto.
Benchi la Ufundi la Azam likiongozwa na Kocha Florent Ibenge, lilifanya mabadiliko ya takribani wachezaji sita kutoka wale wanaoanza mara kwa mara ambapo Fuentes Mendoza na Adolf Mtasingwa walianza baada ya kukaa nje muda mrefu wakiuguza majeraha.
Kiungo James Akaminko ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa akianzia benchi, leo alianza akichukua nafasi ya Himid Mao ambaye alikuwa jukwaani akishuhudia mchezo huo. Vilevile Fei Toto, Mwaikenda na Idd Nado wote walianzia benchi.
Kwenye mechi 30 ilizocheza Azam, imeshinda 17, sare 11 na kupoteza mechi mbili, ikifunga mabao 44 na kuruhusu 12.
Matokeo hayo yameipa heshima Azam iliyomaliza nafasi ya tatu ikiwa na tiketi yake ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, huku Dodoma Jiji iliyopoteza, imekusanya pointi 35 katika nafasi ya tisa.
Hii ni mara ya pili Fei Toto anakosa tuzo ya ufungaji bora katika Ligi Kuu ya NBC akimaliza nafasi ya pili tena baada ya 2023-2024 alipofunga mabao 19, akiwa nyuma ya kinara Stephane Aziz Ki aliyefunga 21.