Prime
MSUVA: Simba, Yanga kituo cha mafanikio au kaburi la vipaji vya wazawa
HEKAHEKA za usajili zinaendelea kushika kasi huku Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni katika kipindi hiki, majina mengi ya wachezaji wazawa yanatajwa kujiunga na vigogo wa soka la Tanzania, Simba na Yanga lakini swali kubwa linabaki kuwa moja; je, watatoboa kwenye vikosi hivyo?
Kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwa na changamoto kwa wachezaji wengi wa ndani kujihakikishia nafasi za kudumu katika vikosi vya Simba na Yanga. Ukianza kuorodhesha majina ya waliowahi kuonekana kuwa na uwezo mkubwa lakini wakashindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, unaweza kubaki na maswali mengi kuliko majibu.
Miongoni mwa wachezaji waliovutia msimu uliopita wa 2024/25 ni Offen Chikola kiungo huyo mshambuliaji alitua Yanga akitokea Tabora United ambayo kwa sasa ni TRA United lakini alishindwa kupata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza na baadaye akaomba kujiunga na Singida Black Stars kwa mkopo.
Akiwa Tabora alifunga mabao saba na asisti mbili, Chikola si wa kwanza kukumbana na hali hiyo, wachezaji wengine ambao wanaendelea kupambania nafasi Yanga ambao waliingia msimu uliopita ni Abdulnassir Mohamed 'Casemiro' na Abubakar Nizar Othman 'Ninju' lakini pamoja na vipaji vikubwa ambavyo wamekwenda navyo kwenye timu hiyo, wanaonekana kuporomoka kila siku na sasa wanachukuliwa kama wachezaji wa kawaida sana na kipindi kingine hata nafasi kwenye benchi hawapati wanaishia jukwaani.
Kwa upande wa Simba, nyota kama Ladack Chasambi, Edwin Balau na wengine kadhaa ambao wametolewa kwa mkopo kama vile Awesu Awesu, Salehe Karabaka naValentino Mashaka wamekuwa na wakati mgumu kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza ni wachache sana ambao wamepenya na kuwa sehemu muhimu ya kikosi pamoja na kwamba walisajiliwa kama wachezaji mahiri huko walipotoka.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za usajili, Simba imefikia makubaliano na Bakari Msimu kutoka Coastal Union, Kelvin Nashon kutoka Pamba Jiji na Nathaniel Chilambo kutoka Azam FC.
Nashon, ambaye ni kiungo mkabaji, atakabiliwa na ushindani mkubwa wa nafasi dhidi ya Yusuph Kagoma na Alassane Kante. Kwa upande wa Chilambo, ambaye ni beki wa kulia, atahitaji kupambana ili kupata nafasi mbele ya mkongwe Shomari Kapombe ambaye ameshawapokea mabeki wengi kwenye eneo lake lakini mwisho wakaondoka na kumuacha akiwa anatamba.
Bakari Msimu mwenye mabao matatu kwenye ligi kwa sasa naye anakwenda kukutana na mtihani mkubwa kama kweli atakuwa ameshamalizana kila kitu na timu hiyo, atakuwa akipigania nafasi katika eneo ambalo tayari lina ushindani mkubwa huku akitarajiwa kuepuka mkasa uliompata Hussein Semfuko aliyesajiliwa kutoka Coastal Union msimu uliopita lakini akashindwa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza pamoja na kwamba alisajiliwa kama mchezaji mkubwa.
Msimu atalazimika kupambana na nyota kama Clatous Chama, Anicet Oura, Libasse Gueye na Elie Mpanzu ambao wanacheza sehemu moja.
Huu ni mtihani mzito kwa kiungo huyo ambaye amekuwa mmoja kati ya nguzo muhimu sana kwenye kikosi cha Coastal Union, amefanya kazi kubwa kwenye michezo yote mikubwa ukiwemo ile ya ligi dhidi ya Yanga, huku amekuwa ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Coastal Union lakini kuna shaka kuwa anaweza kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha Simba endapo atakwenda kwenye timu hiyo kutokana na makocha wengi wa timu hiyo kuamini zaidi kwa wachezaji kutoka nje ya nchi, kama atafanikiwa atailinda nafasi yake kwenye kikosi cha Taifa Stars, lakini akifeli maisha yatakuwa kama ya makinda wengine ambao walijiunga na timu hiyo wakiwa na vipaji vikubwa na sasa wamebaki na heshima tu ya kwamba walikuwa bora huko nyuma.
Kwa upande wa Yanga, taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo imefikia makubaliano na winga wa Fountain Gate, Juma Issa maarufu kama 'Chuga Boy', mwenye mabao mawili kwenye ligi, moja kati ya vipaji vikubwa zaidi kwenye ligi kwa sasa na Yanga wanakumbuka alichofanya kwenye mchezo wao wa ligi juzi.
Winga huyo anaonekana kuwa miongoni mwa vipaji vikubwa vya wazawa kwa sasa, lakini atakutana na ushindani mkali kutoka kwa Pacome Zouzoua, Max Nzengeli na Allan Okello, kwenye jicho la kawaida ni ngumu kwake kutoboa pamoja na kipaji alichonacho.
Kinda huyu amekuwa mwepesi, ana kasi ya hali ya juu ya kupiga chenga na kuuficha mpira, lakini jambo la pekee ambalo kwake pia lipo ni uwezo mzuri wa kupiga mashuti, kumbuka shuti ambalo alipiga langoni mwa Yanga juzi na Djigui Diarra akafanya kazi ya ziada kuokoa.
Ni mmoja kati ya wachezaji wachanga bora kwenye ligi, shida ni kama atatoboa kupata angalau asilimia 50 ya nafasi kwenye kikosi cha Yanga katika nafasi ambayo anacheza, Pacome, Maxi na Okello mmoja akae nje yeye acheze, au ataishia jukwaani kama walivyo Abubakar Nizar Othman 'Ninju', Abdulnasir Abdallah 'Casemiro na Chikola ambao walipotoka walikuwa bora zaidi, wakiwa tegemeo tofauti na sasa.
MSUVA ATOA USHAURI
Nyota hao pamoja na wazawa wengine watakaojiunga na Simba na Yanga wamepewa ushauri na nyota wa zamani wa Yanga, Simon Msuva kuhusu namna ya kufanikiwa katika mazingira hayo yenye ushindani mkubwa.
Msuva, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Al-Talaba SC ya Iraq, alisema siri kubwa ni kutokata tamaa na kuendelea kufanya kazi kwa bidii kila wakati.
"Kuna wachezaji wengi sana wenye vipaji Tanzania, lakini changamoto kubwa huwa ni muendelezo wa kile wanachokifanya. Mpira una mambo mengi sana, unahitaji kufanya zaidi na zaidi bila kuchoka," alisema Msuva.
Aliongeza kuwa kukaa benchi hakupaswi kumvunja moyo mchezaji. "Unaweza kukaa benchi hata mechi 10, lakini ukipata nafasi moja tu unapaswa kuonyesha kwa nini hustahili kubaki nje. Mimi binafsi nilikuwa napenda changamoto, hivyo wanatakiwa kuchukua ushindani wa wachezaji wa kigeni kama chachu ya kufanya vizuri zaidi."
Wakati akiitumikia Yanga, Msuva aliweka historia kwa kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili. Alifunga mabao 17 msimu wa 2014/15 na mabao 14 msimu wa 2016/17, takwimu zilizomfungulia mlango wa kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.