Mlandege yaizamisha KMKM Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Timu ya Polisi inaendelea kutanua mabawa akiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 18 ikitofautiana pointi moja na zinazomfatia ikiwemo JKU yenye 17, Zimamoto 16 na Uhamiaji 15.
JAHAZI la KMKM limezamishwa na timu ya Mlandege baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mechi iliyochezwa uwanja wa Mao A, Unguja.
Ushindi huo unaifanya Mlandege kusogea hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, ikiishusha KMKM nafasi ya nane.
Saidi Matola aliweka kimiani bao la kwanza dakika 28 katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ikienda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja.
Kipindi cha pili cha mchezo huo kilianza kwa kasi ambapo KMKM iliionekana kutaka kusawazisha bao hilo, bila mafanikio huku ikijikuta ikiongezwa la pili na Yussuf Suleiman ‘Jussa’ dakika ya 72.
Katika mchezo mwengine, uliochezwa Oktoba 17, 2026 uwanja wa Gombani uliopo Pemba, Chipukizi iliifunga Fufuni bao 1-0 na kuifanya timu hiyo kupata ushindi wa pili kwenye ligi hiyo baada wa Mlandege.
Kocha Mkuu wa Chipukizi, Suleiman Mohammed ‘Mani Gamera’ aliinoa Fufuni msimu uliopita lakini aliondoka baada ya kutokea sintofahamu kati yake na viongozi wa timu hiyo, kwa kumtuhumu kutopanga kikosi cha ushindani kilichosababisha kufungwa bao 1-0 na Mwenge kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la FA.
Hatahivyo, Licha ya Chipukizi kushinda mechi hiyo bado ipo nafasi ya 13 ya mstari mwekundu ikitoka ya 15 na Fufuni ikiendelea kusalia mkiani mwa msimamo wa ligi.
Timu ya Polisi inaendelea kutanua mabawa akiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikiwa na pointi 18 ikitofautiana pointi moja na zinazomfatia ikiwemo JKU yenye 17, Zimamoto 16 na Uhamiaji 15.