Arjif, Ubwa vita ya Kipa Bora Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Takwimu hizo zinaonyesha namna klabu zilizowekeza kwenye uimarishaji wa safu za beki ili kuhakikisha haitoi nafasi za wazi kwa wapinzani wao.
VITA ya kuwania tuzo ya Kipa Bora Ligi Kuu Zanzibar inazidi kupamba moto baada ya walinda mlango wa timu mbalimbali kuonyesha viwango vya hali ya juu na ushindani wa kutosha.
Katika kinyang'anyiro hicho Kipa wa timu ya Polisi, Arjif Ali Amour anaendelea kushikilia usukani akiwa na cleansheet tano kati ya mechi saba alizocheza.
Arjif amekuwa ngome imara katika lango lake, akionyesha uwezo wa kuongoza safu yake ya ulinzi kwa kuokoa mashambulizi hatari na kuisaidia timu yake.
Kipa huyo alizipata cleansheet hizo katika mechi dhidi ya KVZ, Mwenge, Mafunzo, Mlandege na Raskazone zikimfanya kinara. Hata hivyo, uongozi wa Arjif unapata shinikizo kutoka kwa mpinzani wake wa karibu mlinda mlango wa KVZ, Hamad Ubwa 'Baro' ameingia katika ushindani huo na kujipatia cleansheet sawa na hizo kwenye mechi ya Fufuni, Raskazone, Mlandege, Zimamoto na Kipanga.
Sio Baro pekee anayemfukuzia na anayeleta chachu katika mbio hizo yupo Ahmed Ali Suleiman 'Salula' Kipa wa Uhamiaji, akiwa na michezo nne bila kuruhusu bao.
Mbali na kuwa na uzoefu wa ligi hiyo, Ahmed anaonekana kuwa na utulivu mzuri pindi anapokabiliwa na mashambulizi ya kushtukiza na hizo akizipata kwenye mechi dhidi ya Mwenge, Wembe, Raskazone na Fufuni.
Mbali na hao, Adam Rihaji Shaaban Kipa wa KMKM, Juma Haji Makame wa Raskazone, Rashidi Hamis wa Muembe Makumbi na Nassor Abdalla Nassor wa Chipukizi kila mmoja akiwa nazo tatu.
Ushindani kati ya Arjif, Ahmed na Hamad Ubwa unaendelea kuongoza presha kwa waliopo nyuma yake wanaohitaji kutwaa tuzo hiyo.
Takwimu hizo zinaonyesha namna klabu zilizowekeza kwenye uimarishaji wa safu za beki ili kuhakikisha haitoi nafasi za wazi kwa wapinzani wao.