Mgunda: Mapambano yanaendelea
Muktasari:
- Coastal Union imekuwa na mwendelezo wa matokeo mabovu baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 dhidi Tanzania Prisons katika uwanja wa Nelson Mandela Mkoani Rukwa.
KOCHA wa Coastal Union Juma Mgunda alisema kuwa licha ya timu yake kuwa na mwendelezo mbaya wa matokeo ili mapambano yanaendelea ili kuweza kuinasua timu hiyo kwenye janga la kushuka daraja.
kauli ya Mgunda inakuja baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Nelson Mandela Mkoani Rukwa.
katika mchezo huo uliokuwa wa kasi na kuvutia kwa timu zote mbili ulishuhudia wenyeji Prison wakijiandikia bao la kuongoza kunako dakika ya 19, ya mchezo kupitia kwa Samson Mbangula baada ya kumtoka kipa wa Coastal Union, Abubakar Abas baada ya mabeki wa Coastal Union kudhani mchezaji huyo ameotea.
Licha ya kutanguliwa bao hilo ila Coastal ilirejea mchezoni na kusawazisha bao hilo kunako dakika ya 23 kupitia kwa Abdul Hamis kwa mkwaju wa penati baada ya Marco Mhilu kunawa mpira katika eneo la hatari.
Prison ilijibu mashambulizi ya Coastal kwa kujipatia bao la pili kunako dakika ya 35 ya mchezo kupitia kwa Jeremia Juma baada ya shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Coastal Union, Abubakar Abas.
Hata hivyo Coastal haikukata tamaa kwani ilibidi kusubri mpaka dakika za lala salama kwa kusawazisha bao hilo dakika ya 85 ya mchezo kupitia kwa Mudathir Abdallah aliyeingina kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Raizin Khafidhi aliyeonekana kukosa nafasi za wazi kunako kipindi cha kwanza cha mchezo.
Baada ya mchezo huo kocha wa timu hiyo Juma Mgunda alisema kuwa licha ya mwenendo mbovu wa timu hiyo ila bado mapambano yanaendelea mapaka dakika za mwisho za kuhakikisha timu hiyo inasalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimum ujao.
"Tunatambua umuhimu mkubwa wakuibakisha timu hii kwenye Ligi kuu Tanzania Bara na hii nim kutokana na umuhimu kwa wakazi wetu wa Mkoa wa Tanga, tunajua wazi kuwa sio rahisi kutokana na mwenendo mbovu wa timu yetu ila itoshe tu kusema kuwa tutapambana mpaka dakika za mwisho" alisema Mgunda.
Coastal Union imekuwa na muendelezo mbaya wa matokeo kwani katika mechi 5 zilizopita za timu hiyo kwenye Ligi kuu Tanzania Bara imepoteza michezo 4 na kutoka sare katika mchezo 1.
Coastal Union inasalia katika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 34 katika michezo 31 huku ikisaliwa na michezo mitatu ambayo ni dhidi ya Simba julai 11 kisha Mwadui FC julai 14 na mechi ya mwisho ni dhidi ya Kagera Sugar julai 18.
IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI