Messi vs Ronaldo : Ronaldo afunga kazi Euro2016
TOLEO lililopita, mwandishi, Luca Caioli alizungumzia safu ya ushambuliaji wa Barca ya MSN yaani Messi, Suarez na Neymar ilivyobeba mataji matatu msimu wa 2014/15 na furaha ya Messi msimu uliofuata baada ya kubeba mataji mawili ya La Liga na Kombe la Mfalme. Endelea…
Furaha yake katika mafanikio haya ilikuwa wazi kwenye akaunti yake ya Facebook pale alipoandika, “mabingwa wa La Liga! Tumefanikisha asante kwa juhudi kubwa za kila mmoja wetu, taji hili ni heshima kwa mashabiki wetu ambao wameshikamana nasi hadi mwisho.”
Mbali na kuandika maneno hayo, Messi pia aliambatanisha picha mbili moja ikimuonyesha akionyesha ishara ya ushindi na picha nyingine ya timu nzima ya Barca. Hadi hapo kulikuwa na pigo moja tu kwa Messi, nalo ni kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Barca ilitolewa katika hatua ya robo fainali.
Hali haikuwa hivyo kwa Ronaldo, mpinzani wa kisoka wa Messi ambaye alichukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu katika historia yake ya soka, lakini kubwa zaidi lilikuwa bado halijajitokeza kwa Ronaldo.
Ilikuwa ni mwezi mmoja baadaye, hapana shaka ilikuwa hatua kubwa katika maisha yake ya soka, fainali za Ulaya (Euro 2016) nchini Ufaransa.
Bao lake la kipekee dhidi ya Wales katika hatua ya nusu fainali liliwafungulia mlango wa kuingia katika mtihani wa mwisho dhidi ya wenyeji, Julai 10, 2016.
Timu hizo mbili zilikutana katika dimba la Stade de France mjini Saint Dennis, dakika chache za awali zilipita huku kukiwa hakuna maumivu wala ushindi, lakini kabla dakika 15 hazijapita Ronaldo alichezewa rafu mbaya kwa nyuma na Dimitri Payet.
Mwamuzi hakuiona rafu hiyo na kuruhusu mchezo uendelee lakini hali ilikuwa tofauti kwa Ronaldo, ilijidhirisha wazi wazi kwamba mambo hayakuwa mazuri kwake. Alianza kuchechemea huku akiwa akiushika mguu ulioumia.
Kadri alivyokuwa akijaribu kukimbia uwanjani ilijidhihirisha kwamba Ronaldo alikuwa ameumia na hatimaye alijiangusha chini, madaktari wa timu wakamfunga bandeji kwenye goti na baadaye akarudi uwanjani.
Wachezaji wenzake na nchi nzima ikapumua kwa faraja, ilionekana kama woga. Ronaldo alibeba matumaini ya Ureno kufikia fainali ambayo mwaka 2004 waliipoteza mbele ya Ugiriki.
Ronaldo anapokuwa uwanjani lolote linawezekana na ndio maana dakika chache baadaye akiomba kutolewa na kushindwa kujizuia kulia ilionekana kama Ureno walifikia mwisho wao.
Alitoka nje dakika ya 24 akajivua na kitambaa cha unahodha huku akilia katika hali ya masikitiko makubwa. Gareth Bale, aliingia katika mtandao wa Twitter na kusema kile ambacho wengi walikuwa wakikifikiria, “Inasikitisha kumuona Ronaldo akitoka uwanjani, natumaini hakuna jambo baya sana.”
Bila ya Ronaldo ziliisha dakika 90 bila bao lolote, ni hadithi hiyohiyo katika nusu ya kwanza ya dakika 30 za nyongeza kabla Ederzito Macedo Lopes au Eder hajawa shujaa wa mchezo kwa kuandika bao katika dakika ya 108.
Ronaldo aliyekuwa akichechemea na bandeji mguuni alikuwa amekaa pembeni akifuatilia dakika za mwisho mwisho za mchezo huku akitoa maelekezo kwa wachezaji wenzake.
Filimbi ya kumaliza mchezo ilipopulizwa Ronaldo alirudi uwanjani kwa mara ya tatu lakini safari hii ilikuwa ni kwa ajili ya kushangilia huku akitokwa na machozi zaidi, hatimaye alifanikisha ndoto yake kubwa, kutwaa taji la timu yake ya Taifa.
Bado mafanikio hayo yalikuwa kwake akiwa ndiye nahodha kulibeba taji lililoitangaza Ureno kuwa timu bora ya Ulaya, “wakati wote nimekuwa nikitaka Ureno ishinde kitu kama hiki, iingie katika historia na hatimaye sasa nimeweza, nina furaha.
“Hiki ni kitu ambacho nimekuwa nikikitaka tangu mwaka 2004, hiki ndicho kinachoifaa Ureno, nchi inatakiwa kupata hiki, wakati wote nimekuwa nikiamini kuwa hawa wachezaji wana ujasiri, uwezo na mbinu kutoka kwa kocha wetu za kuifunga Ufaransa na tumeweza.
“Hii ni hatua ambayo haiwezi kusahaulika,” alisema Ronaldo akifahamu kuwa taji hilo ni kitu ambacho wachezaji wachache wameweza kukifanikisha.
Itaendelea Jumamosi ijayo…