Messi,Suarez na Neymar ilipoichapa juve ya kina Pogba
Muktasari:
Suarez aliyetokea upande wa kulia, alichokifanya ni kuugusa kidogo mpira huo, moja kwa moja tu hadi wavuni kuandika bao la pili. Katika dakika za majeruhi, Messi tena alitengeneza nafasi nyingine akamuunganishia Neymar aliyeipatia Barca bao la tatu na ubao kusoma 3-1.
KATIKA toleo lililopita, mwandishi, Luca Caioli aliichambua mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Barca na Juventus ya msimu wa 2014/15. Sasa endelea…
Bao la kwanza lilifungwa na Ivan Rakitic katika dakika ya nne, ni bao la tatu kufungwa kwa kasi katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Lakini Juventus wakapata bao lao baada ya mapumziko, walisawazisha katika dakika ya 55.
Katika dakika 10 zilizofuata walitawala mchezo waliwatia presha wapinzani wao huku mchezo ikiendelea kuwa wenye ushindani.
Katika dakika ya 65, Paul Pogba (kwa sasa anaichezea Man United) aliingia katika eneo la penalti la Barca na katika sekunde chache Juve walikuwa wakiipigania penalti kupitia kwa beki Dani Alves wa Barca lakini penalti hiyo hawakuipata na mpira ukaendelea.
Baadaye Messi akaunasa mpira mbele kidogo ya eneo la kati, akaanza kukimbia kwa kasi na kupiga krosi ambayo kipa wa Juventus, Buffon akaishia kuuparaza mpira hali iliyomuacha Suarez akiwa katika nafasi nzuri.
Suarez aliyetokea upande wa kulia, alichokifanya ni kuugusa kidogo mpira huo, moja kwa moja tu hadi wavuni kuandika bao la pili. Katika dakika za majeruhi, Messi tena alitengeneza nafasi nyingine akamuunganishia Neymar aliyeipatia Barca bao la tatu na ubao kusoma 3-1.
Messi na Barca wakaweka historia, walitwaa taji la La Liga, Kombe la Mfalme na Ligi ya Mabingwa Ulaya, mataji yao matatu kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitano mafanikio ambayo hakuna timu nyingine iliyoyafikia.
Na jambo jingine la kufurahisha ni kwamba safu ya ushambuliaji ya Messi, Suarez na Neymar au MSN katika msimu.
Uwanjani Messi ilionekana kama vile alikuwa tayari amezika tofauti zake na kocha wake, Luis Enrique baada ya kuonekana wakikumbatiana jambo ambalo lilionyesha mabadiliko ndani ya kikosi cha Barca. Hiyo ni baada ya kuanza msimu kwa utata kati ya kocha na mchezaji wake huyo staa hadi kufikia fainali ya kipekee jambo ambalo hakuna ambaye angeweza kulitabiri mwanzoni mwa msimu.
Messi ni kama vile alikuwa amemaliza utata na shutuma zilizoibuka na kurudi katika ubora wa kipekee ambao amekuwa akihusishwa nao.
“Messi amekuwa wa kivutio, ni mchezaji wetu nyota,’’ alisema Enrique katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mechi.
Kwa Messi hilo ni taji lake la nne la Ulaya, ni mafanikio ambayo wachezaji wachache mno wameyafikia na kesho yake kukawa na picha kwenye mitandao ikimuonyesha akipata mlo wa asubuhi akiwa na kombe.
Akiwa katika kufurahia taji hilo na mashabiki Nou Camp, Messi anakumbukwa kusema, Tutaendelea na kasi hii, tuna hasira na tunataka kuendelea kushinda,’’ alionekana akitabasamu wazi wazi, akifurahia mafanikio waliyofikia.
Miezi 12 baadaye yaani msimu wa 2015/16, Messi alisababisha furaha kwa mara nyingine, safari hii hakukuwa na kushiriki fainali tatu msimu mmoja, lakini Barca ilibeba mataji mawili makubwa, La Liga na Kombe la Mfalme.
Furaha yake katika mafanikio haya ilikuwa wazi kwenye akaunti yake ya Facebook pale alipoandika, “Mabingwa wa La Liga!!! Tumefanikisha asante kwa juhudi kubwa za kila mmoja wetu, taji hili ni heshima kwa mashabiki wetu ambao wameshikamana nasi hadi mwisho.”
Mbali na kuandika maneno hayo, Messi pia aliambatanisha picha mbili moja ikimuonyesha akionyesha ishara ya ushindi na picha nyingine ya timu nzima ya Barca .
Hadi hapo kulikuwa na pigo moja tu kwa Messi katika msimu wa 2015/16, nalo ni kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Barca ilitolewa na Atletico Madrid katika hatua ya robo fainali.
Itaendelea Jumanne ijayo…