Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City yatakata Sokoine ikiichapa Dodoma Jiji

Muktasari:

  • Mbeya City, ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja kupitia mechi za mchujo (play-off), ilianza msimu huu kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold.

Baada ya kuanza vibaya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, Mbeya City imefufua matumaini yake ya kufanya vizuri baada ya kuichapa Dodoma Jiji mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mbeya City, ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja kupitia mechi za mchujo (play-off), ilianza msimu huu kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold.

Kwa upande wa Dodoma Jiji, ilianza kampeni yake kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, kabla ya kukutana na kipigo chake cha kwanza msimu huu mbele ya Mbeya City.

Katika mchezo huo uliochezwa saa 8:00 mchana, wenyeji Mbeya City walionyesha kiwango kizuri, wakishambulia kwa kasi huku wakiwa imara katika eneo la ulinzi na kuwadhibiti wapinzani wao.

Willy Mwani aliipa Mbeya City bao la kuongoza dakika ya tisa, akimalizia vizuri shambulizi la wenyeji na kulifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Mbeya City ilipata nafasi kadhaa za kuongeza bao kabla ya mapumziko, lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia.

Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji kuendelea kutafuta bao la pili, juhudi ambazo zilizaa matunda dakika ya 78 baada ya Yahya Mbegu kuandika bao la pili kwa shuti lililomshinda kipa wa Dodoma Jiji, Ally Salim.

Pamoja na kupoteza mchezo huo, Dodoma Jiji haikuwa timu ya kubezwa kutokana na namna ilivyomiliki mpira na kuonyesha soka zuri, lakini ukosefu wa umakini katika eneo la mwisho uliigharimu.

Kipa wa Mbeya City, Toba Kutusha, alikuwa miongoni mwa waliofanya kazi kubwa kuhakikisha timu yake inaondoka na pointi zote tatu, akifanya uokozi muhimu katika dakika za mwisho baada ya Dodoma Jiji kupata nafasi mbili za hatari.


Mashami: Tumekosa umakini

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Vincent Mashami, amekiri timu yake ilicheza vizuri lakini ikakosa umakini katika eneo la mwisho, huku makosa binafsi yakiwapa wenyeji nafasi ya kuibuka na ushindi.

“Tumemiliki mpira, lakini tatizo limekuwa katika umaliziaji. Yapo makosa binafsi yaliyofanyika, ila tunaenda kuyasahihisha ili kwenye mchezo ujao nyumbani tufanye kweli,” alisema Mashami.


Mayanga: Tunaenda kuboresha

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema licha ya ushindi huo, bado ana kazi ya kuboresha safu yake ya ushambuliaji kutokana na nafasi nyingi walizopata lakini hawakuzitumia ipasavyo.

“Tunaenda kuboresha na kusahihisha katika mchezo ujao dhidi ya Mashujaa. Leo vijana wamefanya vizuri na tumepata mchezo mzuri.

“Tunahitaji kuendeleza makali haya kwa sababu ligi ni ngumu na hatukuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa,” alisema Mayanga.