Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Julietha Singano amfuata Luvanga Al Nassr

Muktasari:

  • Singano anajiunga na kikosi hicho akiwa Mtanzania wa pili ndani ya timu hiyo kusajiliwa baada ya Clara Luvanga ambaye amekuwa sehemu ya Al Nassr kwa takribani misimu mitatu sasa.

BEKI wa Mtanzania Julietha Singano amejiunga na Al Nassr Women ya Ligi Kuu ya Wanawake Saudia kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Juarez ya Mexico.

Singano anajiunga na kikosi hicho akiwa Mtanzania wa pili ndani ya timu hiyo kusajiliwa baada ya Clara Luvanga ambaye amekuwa sehemu ya Al Nassr kwa takribani misimu mitatu sasa.

Beki huyo wa timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, amesajiliwa baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa Mexico, jambo lililowashawishi mabosi wa Al Nassr kumuongeza katika kikosi hicho kwa ajili ya msimu wa 2026-2027.

Chanzo kiliambia Mwanaspoti kuwa, tayari Singano yupo nchini Saudia na kilichobaki ni kumtambulisha kwani ameshashiriki baadhi ya matukio ya timu hiyo. “Kulikuwa na ofa tatu za Saudia ambazo ni Al Ittihad, Nasr na Al Hilal zote zikimuhitaji, lakini mabingwa hao watetezi waliweka mpunga mrefu, Singano akasaini huko na kila kitu tayari bado kumtambulisha,” kilisema chanzo hicho.

Singano alijiunga na Juarez ya Mexico katika msimu wa 2022-2023 akitokea Simba Queens, tangu wakati huo amekuwa mmoja wa mabeki tegemeo wa timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kucheza mechi nyingi na kuhimili ushindani wa ligi.

Singano ambaye alikuwa beki tegemeo wa Juarez akionyesha uimara tangu alipojiunga na klabu hiyo, alifanikiwa kucheza jumla ya mechi 103 za ligi.

Katika kipindi hicho, beki huyo alionyesha mchango katika kulinda safu ya ulinzi lakini pia amekuwa akisaidia timu yake kwenye mashambulizi, akifunga mabao mawili na kutoa asisti nne.

Msimu wa 2025-2026, Singano alicheza mechi 26, akifunga bao moja na kutoa asisti moja huku akionyeshwa kadi tano za njano.

Msimu wa 2024-2025 uliendelea kuwa mzuri kwake baada ya kucheza mechi 33 akifunga bao moja, asisti moja.

Katika msimu wa 2023-2024, alicheza mechi 30 bila kufunga bao, lakini alitoa asisti tatu.

Takwimu hizo zilimfanya kuwa mchezaji muhimu katika safu ya ulinzi ya Juarez lakini kwenye ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.

Ubora huo ulimfanya kutajwa mara kadhaa kama nyota mwenye mchango mkubwa kikosini.

Singano sasa anaungana na Mtanzania mwenzake Clara Luvanga ambaye amekuwa sehemu ya kikosi hicho kwa misimu mitatu.

Mbali na Singano na Luvanga, Mtanzania mwingine aliyewahi kukipiga kwenye ligi hiyo ni kiungo mshambuliaji Enekia Lunyamila aliyetambulishwa Querétaro Femenil ya Mexico.