Mayanga asisitiza jambo Mbeya City
Muktasari:
- Amesema matokeo yaliyotokea msimu uliopita hawataki yajirudie, akieleza kuwa ili kutimiza malengo ni lazima wapambane mechi za mzunguko wa kwanza kusaka ushindi kujiweka salama mapema katika ligi hiyo.
ACHANA na ushindi walioupata Mbeya City katika mechi iliyopita, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amesema njia ya kuepuka aibu na presha za kushuka daraja ni lazima wakusanye pointi nyingi mapema.
Amesema matokeo yaliyotokea msimu uliopita hawataki yajirudie, akieleza kuwa ili kutimiza malengo ni lazima wapambane mechi za mzunguko wa kwanza kusaka ushindi kujiweka salama mapema katika ligi hiyo.
Msimu uliopita timu hiyo iliponea chupuchupu kushuka daraja kupitia play off, ambapo msimu huu tayari imeshinda mchezo mmoja kati ya miwili iliyocheza na kuwa nafasi ya sita.
Timu hiyo pekee Ligi Kuu katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, katika mechi mbili ilizoanza nazo, imepoteza mmoja dhidi ya Geita Gold kabla ya kushinda mbele ya Dodoma Jiji na sasa itakuwa kibaruani tena dhidi ya Mashujaa nyumbani jijini Mbeya.
Mayanga amesema namna bora ya kuepuka presha ya dakika za mwisho ni kutafuta ushindi kwa mechi za raundi ya kwanza, ambazo zitawaweka pazuri kabla ya kuanza kukimbizana mwishoni. Amesema wachezaji wanalo jukumu la kupambana kila mchezo kuhakikisha wanapata pointi tatu akieleza kuwa kiwango walichoonesha kinatoa matumaini ya kufanya vizuri.
“Lazima tupambane kutafuta ushindi kwenye mechi hizi za mwanzo kabla ya kuanza presha mzunguko wa pili ambapo ligi inakuwa imeanza kuchanganya, kimsingi vijana wameonesha mwanzo mzuri.
“Ha tupaswi kubweteka wala kuridhika haraka bali tujitahidi kutafuta ushindi kwenye hizi mechi za mwanzo, tukifanikiwa tutaondokana na presha za dakika za mwisho kama ilivyokuwa msimu uliopita,” amesema Mayanga.
Kocha huyo hakusita kuitaja safu ya ushambuliaji kutotumia nafasi wanazopata, akieleza kuwa ipo kazi inahitajika kufanyika kuipa makali zaidi ili kufikia malengo yao msimu huu.
Kwa upande wake kipa wa timu hiyo, Nelson Oden, amesema matarajio yao ni kuiweka nafasi nzuri licha ya ugumu wa ligi hiyo akibainisha kuwa kiu ya wachezaji ni kufanya vizuri kila mchezo.
“Pamoja na kwamba ni msimu wangu wa kwanza kucheza Ligi Kuu lakini naiona Mbeya City tukifanya vizuri kwakuwa kila mchezaji anao uwezo na shauku ya kufikia malengo, lazima tujitoe kwa faida yetu na timu kwa ujumla,” amesema.