Baraka Mwangosi aibukia Polisi Tanzania
Muktasari:
- Taarifa ilizozipata Mwanaspoti, Simba ilipokuwa inafanya mchakato wa kumsajili Ismail Mgunda, uongozi wa Mashujaa uliomba huduma ya Mwangosi, lakini mchezaji huyo alichagua kwenda Polisi Tanzania.
MSHAMBULIAJI Baraka Mwangosi, amejiunga na Polisi Tanzania, iliyomsajili kwa mkopo kutoka Simba ambako hakuwa na nafasi kubwa ya kuanza moja kwa moja kikosi cha kwanza.
Taarifa ilizozipata Mwanaspoti, Simba ilipokuwa inafanya mchakato wa kumsajili Ismail Mgunda, uongozi wa Mashujaa uliomba huduma ya Mwangosi, lakini mchezaji huyo alichagua kwenda Polisi Tanzania.
Kuhusu kutakiwa na Mashujaa, meneja wa timu hiyo, Athuman Athuman, alikiri ni kweli walihitaji huduma yake akisema: “Kumtaka mchezaji ni jambo lingine, kumpata ni hatua nyingine.”
Alipotafutwa Mwangosi ili kuzungumzia uhamisho wake wa kwenda Polisi Tanzania, amesema: “Muda utaongea nikianza kuonekana uwanjani, ila kwa sasa sina la kuzungumza.”
Simba ilimsajili Mwangosi kupitia dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Mbeya City baada ya kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Uhamisho huo wa kwenda kucheza kwa mkopo, aliuzungumzia staa wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel akisema: “Ni kitu kizuri kwake kwenda kupata uzoefu na nafasi ya kucheza, upambanaji wake utampa nafasi ya kurejea, lazima ajue kucheza ni bora zaidi kwani kutapandisha kiwango chake na kumjengea kujiamini.”