Simba dhidi ya Pamba na kumbukumbu ya sare iliyotibua hesabu
Muktasari:
- Pamba Jiji ilivuruga hesabu za Simba katika mechi ambayo iliongeza presha katika mbio za ubingwa huku timu hiyo ikimaliza msimu ikiwa pointi mbili nyuma ya Yanga iliyotwaa taji kwa mara ya tano mfululizo ikiwa na pointi 75.
MIONGONI mwa timu zilizowahi kuitibulia Simba hesabu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita ni Pamba Jiji, ambayo ililazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza siku 154 zilizopita, sawa na miezi mitano na siku moja.
Pamba Jiji ilivuruga hesabu za Simba katika mechi ambayo iliongeza presha katika mbio za ubingwa huku timu hiyo ikimaliza msimu ikiwa pointi mbili nyuma ya Yanga iliyotwaa taji kwa mara ya tano mfululizo ikiwa na pointi 75.
Simba leo saa 10:15 itarejea CCM Kirumba, ikiwa na dhamira ya kuendeleza mwanzo mzuri wa msimu mpya chini ya Kocha Steve Barker, baada ya kuanza kampeni kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba.
Kwa upande wa Pamba Jiji, mchezo huo utakuwa wa kwanza wa msimu mpya mbele ya mashabiki wake wa Mwanza huku kikosi hicho kikisaka ushindi wa kwanza baada ya kuanza ligi kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji.
Ingawa Simba iliichapa Pamba Jiji mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Juni 14, 2026, sare ya mchezo wa kwanza bado ni sehemu ya kumbukumbu za msimu uliopita ambapo Simba ilipoteza pointi 14 katika michezo ya aina hiyo.
Kwa jumla, Simba ilitoka sare katika michezo saba msimu uliopita, jambo lililokuwa miongoni mwa sababu zilizofanya ishindwe kutwaa ubingwa licha ya kumaliza na pointi 73, tofauti ya pointi mbili dhidi ya mabingwa Yanga.
Barker amekiri mchezo wa leo hautakuwa mwepesi huku akitaja mambo mawili, ubora wa uwanja pamoja na maandalizi ya Pamba Jiji kuwa miongoni mwa mambo ambayo Simba inapaswa kuyazingatia kabla ya mchezo huo.
“Tunajua ubora wa uwanja, pia tunajua mpinzani atafanya kila kitu kuhakikisha anatuzuia kupata matokeo tunayoyataka. Lakini sisi tumejiandaa kwa hilo na tunahitaji kuhakikisha tunatumia taarifa tulizonazo kuhusu wapinzani wetu ili kutengeneza mpango mzuri wa mchezo,” amesema Barker.
Kocha huyo amesema kikosi chake kinaendelea kuimarika kadiri msimu unavyoendelea, akieleza kuwa maandalizi ya Simba kabla ya kuanza kwa ligi hayakuwa mazuri kutokana na changamoto za kupata muda wa kutosha wa kukifanyia kazi kikosi kizima.
“Ni mchakato wa kuendelea kuboresha timu. Nimesema mara kadhaa katika wiki hizi kwamba tunahitaji kuendelea kuwa bora kadiri msimu unavyoanza. Tulikuwa na maandalizi magumu kabla ya msimu hasa kwa upande wa uwezo wa kukifanyia mazoezi kikosi kizima, lakini kila mchezo unatupa nafasi ya kuimarika zaidi,” amesema.
Barker ameongeza kuwa maendeleo hayo hayataonekana kwenye upande wa nguvu za mwili pekee, bali pia katika namna timu inavyotekeleza mipango yake ya kiufundi uwanjani, akiamini kila mchezo utawafanya wachezaji wake kuwa bora zaidi.
“Kadiri michezo inavyoendelea, tutakuwa imara zaidi kimwili na pia kiufundi. Tunataka kuendelea kujenga timu ambayo itaelewana vizuri na kutekeleza kile tunachotaka ndani ya uwanja,” amesema.
Kwa upande mwingine, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji FC, Francis Baraza amesema anatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na ubora wa Simba lakini amesisitiza kuwa kikosi chake kimejiandaa kupambana na kufanya vizuri mbele ya mashabiki wake.
“Tunafahamu ni mechi ngumu kwa sababu tunacheza dhidi ya timu kubwa yenye wachezaji wazuri, lakini tumejiandaa kwa ajili ya mchezo huu. Tunawaheshimu Simba, lakini pia tunaamini katika uwezo wa kikosi chetu na tunataka kufanya vizuri mbele ya mashabiki wetu,” amesema Baraza.
Wakati macho ya mashabiki wengi yakielekezwa CCM Kirumba, mechi nyingine zitapigwa leo katika Ligi Kuu Bara, ikiwamo ya Mbeya City dhidi ya Dodoma Jiji, huku wenyeji wakiwa wanatafuta kujinasua baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza kwa kufungwa bao 1-0 na Geita Gold.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Kagera Sugar na Singida Black Stars, ambapo wenyeji wataingia uwanjani wakitaka kurekebisha makosa baada ya kuanza msimu kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Simba, Singida ikianza kwa kuichapa Fountain Gate mabao 3-0.